• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Thierry Henry ajiondoa kwenye mitandao ya kijamii kulalamikia ongezeko la visa vya ubaguzi wa rangi

Thierry Henry ajiondoa kwenye mitandao ya kijamii kulalamikia ongezeko la visa vya ubaguzi wa rangi

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Arsenal na Ufaransa, Thierry Henry, amejiondoa kwenye akaunti za mitandao yote ya kijamii kutokana na ongezeko la visa vya ubaguzi wa rangi katika majukwaa hayo.

Henry, 43, aliwaarifu mashabiki wake milioni 2.3 kwenye mtandao wa Twitter kuhusu maamuzi yake hayo mnamo Ijumaa akisema “visa vya ubaguzi wa rangi mitandaoni vimefikia kiwango cha kutisha kiasi cha kutopuuzwa tena”.

Kwa mujibu wa Henry, yeye hatarejea tena kwenye mitandao ya kijamii hadi wakati ambapo kampuni zinazomiliki majukwaa hayo “zitakapoanza kukabiliana na suala la ubaguzi wa rangi kwa kiasi sawa na jinsi wanavyopigana na tatizo la kukiukwa kwa haki za umiliki”.

Henry aliongoza Arsenal kujitwalia mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alipokuwa mchezaji wa kikosi hicho kati ya 1999 na 2007.

Mnamo Septemba 2020, Henry alifafanua baadhi ya nyakati ambapo alipitia masuala ya ubaguzi wa rangi akivalia jezi za Arsenal nchini Uingereza na alipokuwa akiwajibikia timu yake ya taifa ya Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sitagura Liverpool hata tukishindwa kufuzu UEFA muhula ujao...

Aina hatari zaidi ya corona yagunduliwa TZ