• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Ajabu mwanamume kupatikana akifukua kaburi la mkewe Nakuru

Ajabu mwanamume kupatikana akifukua kaburi la mkewe Nakuru

NA JOHN NJOROGE

POLISI eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru wanachunguza kisa ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 43 alipatikana akifukua mwili wa mkewe aliyefariki na kuzikwa Februari 2023 katika kijiji cha Munyukwa, Lokesheni ya Ndoswa.

Jamaa huyo alipatikana akifukua mwili huo mnamo Jumapili Oktoba 15, 2023.

Akithibitisha kisa hicho, Chifu wa eneo hilo Jonnah Komen alisema alipata taarifa kutoka kwa wake – naibu chifu, Haron Koima ambaye alikuwa ametembelea nyumba ya mshukiwa baada ya kuarifiwa na umma.

“Msaidizi wangu alitishiwa na mtuhumiwa kwa silaha hatari, akanipigia simu kunifahamisha kuhusu tukio hilo. Muda mfupi baadaye, mmoja wa watoto wa mtuhumiwa alinijulisha kuwa baba yake alikuwa akifukua kaburi la mama yao katika hali isiyoeleweka,” alisema Chifu Komen.

Jamaa aliyepatikana akifukua kaburi la mkewe Nakuru akipelekwa katika Kituo cha polisi cha Elburgon. PICHA|JOHN NJOROGE

Alifichua kwamba mshukiwa alikuwa akiishi peke yake, baada ya kufukuza wanawe mkewe alipofariki.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, Chifu Komen alisema jamaa huyo alikamatwa kupitia usaidizi wa machifu wenzake, wanachama wa Mpango wa Nyumba Kumi na raia.

“Alipogundua kuwa tunamtafuta alitorokea katika shamba la mahindi ya jirani, lakini tulifanikiwa kumkamata. Tulimpeleka katika Kituo cha Polisi cha Elburgon ambapo anazuiliwa akisubiri kufunguliwa mashtaka kortini,” alisema.

Inasemakana mwanamume huyo hakuwa akielewana na majirani.

Mkazi aliyeomba kubana majina yake, alisema mwanamume huyo alijiunga na dhehebu fulani ambalo huenda lilishiriki kumpotosha.

“Tunaamini uchunguzi wa polisi utabaini ukweli wa mambo kuhusu mienendo yake,” alisema.

Chifu wa Ndoswa Jonnah Komen (kushoto) akiwa na Chifu Msaidizi wa Kapcholola, Kenneth Rotich walipomkamata mshukiwa aliyepatikana akifukua kaburi la mkewe aliyefariki Februari 2023 katika kijiji cha Munyukwa, Kaunti Ndogo ya Molo, Nakuru mnamo Oktoba 15, 2023. PICHA|JOHN NJOROGE

Chifu Komen alisema kesi yake tayari imetwaliwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI), ili kubaini sababu ya kutaka kufukua mwili wa mkewe marehemu.

Kaburi la mwendazake lilikuwa limefukuliwa nusu, huku msalaba ukiwa umewekwa kando kabla kulifunika tena.

Chifu Komen alisema vifaa kama vile jembe, shoka na koleo vilivyopatikana kwenye kaburi hilo, vitasaidia polisi kufanya uchunguzi.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke Uingereza ajioa mwenyewe baada ya kukosa mume

Eneo Kiambu ambapo vijana hawavuti bangi, kunywa pombe wala...

T L