• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Alishwa kifungo cha miezi 36 jela kwa kutusi mkewe

Alishwa kifungo cha miezi 36 jela kwa kutusi mkewe

NA TITUS OMINDE

MWANAMUME Eldoret amehukumiwa kifungo cha miezi 36 gerezani baada ya kupatikana na hatia kutumia mkewe jumbe zenye cheche za matusi.

Fidel Ochieng Mbinda, Jumatatu, Julai 24, 2023 alipokezwa kifungo hicho na Mahakama ya Eldoret baada ya kukiri kosa la kutuma jumbe za matusi kwa mke, Bi Sharon Bwonya, waliyekosana.

Mshtakiwa alihukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 36 jela au kulipa faini ya Sh100, 000.

Bw Mbinda alipatikana na hatia ya unyanyasaji wa kimtandao, kinyume na kifungu cha 27 cha sheria ya matumizi ya tarakilishi na uhalifu wa mtandao ya 2018.

Mahakama iliambiwa kwamba kati ya Julai 10 na 19, 2023 Mjini Eldoret, alitumia simu yake ya rununu kutuma ujumbe wa kuudhi kwa Bi Bwonya.

Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa maneno yaliyotumwa na mshtakiwa yalikuwa machafu sana kiasi kwamba karani wa mahakama aliona aibu kuyasoma mahakamani.

Hati ya mashtaka ilionyesha kuwa mshtakiwa hakuwa na heshima kwa mke wake ambaye walikosana naye pamoja na babake ambaye ni kasisi mkuu katika kanisa moja mjini Eldoret.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Eldoret Nancy Barasa alibainisha kuwa maneno yaliyotumiwa na mshtakiwa yalijaa uchafu na kukosa heshima kwa mlalamishi na wazazi wake.

Mahakama pia ilisema kuwa mshtakiwa alipita mpaka kwa kuwadhulumu wazazi wa mkewe ambao hawakuwa sehemu ya mgogoro wao.

“Tofauti zako za kibinafsi na mke wako hazikuwa kibali cha wewe kukosa heshima kwa baba na mama mkwe. Ukiwa kijana mkwe unatarajiwa kuwaheshimu wazazi wako bila kujali hali,” Hakimu alisema alipokuwa akitoa hukumu hiyo.

Wakili wa serikali Jairus Onkoba aliambia mahakama kuwa ni jamboa la kudunisha kwa kijana mkwe kutoa maneno machafu na ya matusi kwa mkewe na wa wazazi wake.

Bw Onkoba alisema mshtakiwa alikosa heshima kwa walalamishi na imekuwa mtindo wa kawaida, hasa kwa watu walio na uhusiano mbaya kutupiana cheche za matusi kupitia kwa simu zao.

Aliitaka mahakama kumpatia mshtakiwa adhabu kali ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Katika malilio yake, mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa alijutia alichokifanya na ni kutokana na hisia baada ya kugundua kuwa mkewe alifuata ushauri wa wazazi wake wa kutengana naye.

“Ninajutia nilichofanya, ilitokana na hisia baada ya kugundua kuwa nimeachwa na mwanamke niliyempenda sana kutokana na ushawishi wa wazazi wake,” aliambia mahakama.

Hakimu alisema maneno yaliyotamkwa na mshtakiwa ni ya aibu na kiburi, na hayatakiwi hasa katika jamii ya Kiafrika.

“Hata kama ulikuwa umelemewa na hisia, maneno uliotumia ni machafu, yenye matusi na hayana heshima kwa wazazi wa mwanamke unayedai kumpenda,” Hakimu akasema, akitoa hukumu.

Mshtakiwa ana siku 14 kukata rufaa.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Granton Samboja arudi kwa utangazaji redioni

Wakili Ndegwa Njiru: Polisi Watamu walikuwa wanasubiri amri...

T L