• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Aliua mwanawe ili apate nafasi ya kuyoyomea Uarabuni lakini sasa atatumikia kifungo cha miaka 10 jela

Aliua mwanawe ili apate nafasi ya kuyoyomea Uarabuni lakini sasa atatumikia kifungo cha miaka 10 jela

NA PHILIP MUYANGA

MWANAMKE mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kwa kumuua mwanawe wa mwaka mmoja na kumtupa kisimani ili aweze kusafiri Arabuni.

Jaji Anne Ong’injo wa Mahakama Kuu ya Mombasa alisema kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha kesi yake dhidi ya mwanamke huyo Bi Happy Mwenda Mumba.

Jaji huyo pia alisema kuwa mshtakiwa anafaa kuadhibiwa sio tu kuonya wengine, lakini kumfahamisha ya kuwa maisha ni matakatifu na mwanawe alikuwa na haki kikatiba, kuishi.

“Mahakama imezingatia ya kuwa mtoto asiyekuwa na hatia anayemtegemea mshtakiwa alifariki kwa sababu ya maslahi ya kibinafsi ya mshtakiwa. Alimuua ili aweze kusafiri UAE,” alisema Jaji Ong’injo.

Katika uamuzi wake, jaji alisema kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ya kuwa mshtakiwa alikuwa amehusika na kifo cha mwanawe wa kiume haukupingwa na taarifa ya mshtakiwa iliyotolewa bila kiapo mahakamani.

Jaji Ong’injo alisema kuwa marehemu alikuwa mtoto wa mwaka mmoja na alikuwa akimtegemea mshtakiwa kumlinda kutoka kwa hatari yoyote kwa kuwa alikuwa mzazi pekee kwake (marehemu).

“Mshtakiwa chini ya giza alimweka majereha mtoto akiwa na nia ya kumsabishia majeraha mabaya, na kuhakikisha ya kuwa hatanusurika alimtupa ndani ya kisima cha futi kumi,” alisema jaji huyo.

Jaji Ong’injo alisema kuwa vile kitendo hicho kilivyotekelezwa ni thibitisho ya kiwango cha uovu kwa upande wa mtekelezaji.

Mahakama ilisema kuwa mshtakiwa alisemekana kuwa alikuwa ameenda kwa mafunzo akiwa na nia ya kusafiri UAE na kwamba mtoto ndiye aliyekuwa pingamizi na akaamua ammalize.

“Kwa hivyo mshtakiwa amepatikana kuwa alitekeleza kinyume cha sheria kitendo hicho ambacho kilisababisha kifo cha marehemu,”alisema jaji Ong’injo.

Kabla ya kufungwa,mshtakiwa aliyekuwa ameomba mahakama imsamehe akisema kuwa alikuwa ni mkosaji wa kwanza na alikuwa ni mama ya watoto wengine wawili.

Mshtakiwa alitekeleza kitendo hicho mnamo Julai 7 mwaka jana katika eneo la Bombo, kaunti ndogo ya Kisauni, Mombasa. Mashahidi wanane walitoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa.

  • Tags

You can share this post!

Kwani unatumia simu ya ‘katululu’? DJ Mo azushia polisi...

Rooney afanyiwa ‘ile kitu’ sasa yeye ni gumegume bila...

T L