• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Anaamini talanta ya kuigiza itasaidia wengi miaka ijayo

Anaamini talanta ya kuigiza itasaidia wengi miaka ijayo

Na JOHN KIMWERE 
ANASEMA kuwa amepania kujituma katika masuala ya uigizaji huku akilenga  kuibuka produsa tajika ndani ya miaka mitano ijayo.
Beth Njoki Ng’ang’a maarufu Sunshine ni mwigizaji chipukizi ambaye pia hujihusisha na masuala  ya urembo. ”Ndio nimeanza kupiga ngoma lakini ninaamini ninatosha mboga kushiriki masuala ya maigizo,” binti huyu alisema na kuongeza kuwa tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa mwigizaji.
Kando na kwamba alitamani kuwa uigizaji akiwa mtoto anasema filamu ya Nairobi Half Life ilimchochea zaidi kujituma katika masuala ya maigizo. Pia anadokeza kuwa alivutiwa na mwigizaji mahiri hapa nchini Nice Wanjeri maarufu kama Shiru aliyepata umaarufu kutokana na kipindi cha Auntie Boss kilichokuwa kinapeperushwa kupitia NTV.
Dada huyu anasema angependa sana akuze talanta yake katika masuala ya uigizaji anakolenga uibuke tengemeo kuu maishani mwake. Kisura huyu anasema kuwa amepania kushiriki uigizaji huku akifuata nyayo zake mwigizaji mahiri duniani Taraji Penda Henson mzawa wa Marekani maarufu kama Cookie.
Msanii huyo anajivunia kushiriki filamu kama ‘Empire,’ ‘What men want,’ ‘Baby boy,’ na ‘Hidden figures’ kati ya zinginezo. Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1999 katika Kaunti ya Kiambu anajivunia kufanya kazi na makundi kadhaa ikiwamo White Rhino, Zamradi Production na Hoods Creations.
Beth Njoki Ng’ang’a maarufu Sunshine Picha/JOHN KIMWERE
 Amefanikiwa kushiriki filamu za Centro Cinema ambazo hupeperushwa kupitia Inooro TV pia filamu ya Kina ambayo huonyeshwa kupitia Maisha Magic East.  Kwa waigizaji wa humu nchini anasema angependa kufanya kazi na Kate Actress na  Wilbroda walioshiriki Mother Inlaw na Papa Shirandula mtawalia.
Anataka serikali ianzishe sheria zitakaolinda wasanii wote kwa jumla (msanii wa hadhi ya juu pia yule wa kiwango cha chini).  Anashikilia kuwa serikali inastahili kuwekeza zaidi katika sekta ya uigizaji na kuwaunga mkono wasanii wanaoibukia bila kusahau kuanzisha vituo husika katika kila Kaunti.
”Ninawaomba waigizaji waliotutangulia watushike mikono, wakuze talanta pia watuonyeshe mwekeleo kwa ajili ya kutwaa nafasi zao watakapoondoka duniani.” Anasisitiza kuwa wenzao waliowatangulia kwenye gemu hupenda kupuuza wasanii wanaokuja ilhali wanafahamu hawataishi milele.
 
CHANGAMOTO
Bila shaka tasnia ya uigizaji imevufika pandashika nyingi tu.  ”Ikiwa ni ndani ya muda mchache tu nimekubana na pandashuka nyingi,” alisema. Alidokeza kuwa nyakati zingine hufanya kazi na malipo kucheleweshwa.
”Pia nimekutana na maprodusa wengi ambao hupenda tuwe na mahusiano ya kimapenzi ndipo wanipe ajira,” akasema.
USHAURI
Anashauri wenzie kuwa wafahamu safari ndefu huanza kwa hatua moja wajiheshimu, wajipende pia wazingatie sababu ya kujiunga na uigizaji wala wasiwe wepesi wa kutafuta sifa.
Pia anawaambia wakomae aste aste maana wakija kwa pupa katika tasnia ya uigizaji hawatafika popote.
  • Tags

You can share this post!

Griezmann ashindwa kung’aa katika mechi ya kwanza ya...

Waliong’ara NSL watuzwa