• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Anita: Analenga kutesa katika uigizaji na masuala ya urembo

Anita: Analenga kutesa katika uigizaji na masuala ya urembo

Na JOHN KIMWERE 
NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika sanaa yake na kutambulika kote duniani. 
 Anita Wanjiru Njoroge maarufu kama Anita ni miongoni mwa wasanii chipukizi wanaolenga kupata umaarufu si haba hapa nchini pia kimataifa huku wakipania kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.
Msichana huyu aliyezaliwa mwaka 2001 kwa sasa ni  mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Taasisi iitwayo Saki anakosomea kuhitimu kwa shahada ya Diploma katika masuala ya urembo.
Ingawa hajapiga hatua kubwa katika masuala ya maigizo anasema analenga kushiriki filamu zilizo na mafunzo kuhusu masuala mbali mbali ya kimaisha akilenga kushinda tuzo tofauti hapa nchini na kimataifa.
”Nilianza kujihusisha na masuala ya maigizo mwaka 2016 nikisoma Shule ya Upili mwaka 2017 baada ya kuvutiwa na kazi ya makundi mbali mbali yaliokuwa yakizuru shuleni mwetu,” amesema.
Msanii chipukizi, Anita Wanjiru Njoroge… Picha/JOHN KIMWERE
”Ingawa ndio mwanzo nimeanza kupiga ngoma ninaamini ninazidi kujifunza mambo mbali mbali katika tasnia ya uigizaji,”  binti huyu akasema na kuongeza kuwa ana imani atafikia kiwango anacholenga katika jukwaa la filamu.
Anasema alikuwa akishiriki filamu za kutumia mwongozo wa vitabu vya riwaya chini ya kundi liitwalo Path Finders. Chipukizi huyu anajivunia kushiriki kipindi cha  Perfect Match hivi karibuni ambacho kilipeperushwa kupitia Ebru TV mwaka uliyopita.
”Kusema ukweli nafasi ya kushiriki kipindi hicho ilinitia motisha zaidi ikiwa mara ya kwanza kazi  yangu kuonyeshwa kwenye runinga,” alisema na kuongeza kuwa amepata ujasiri wa kushiriki kazi ya uigizaji bila kuhofia lolote wala kuvunjika moyo.
Kisura huyu anasema tangia akiwa mdogo alitamani kuhitimu kuwa mwanahabari wa Televisheni pia msusi. Katika mpango mzima anasema ndani ya miaka mitano ijayo analenga kujituma kwa udi na uvumba kuhakikisha ameshiriki zaidi ya filamu kumi na kufaulu kupeperusha kwenye runinga.
Kwa waigizaji wa kimataifa dada huyu anasema angependa sana kufikia hadhi ya Mercy Johnson mzawa wa Nigeria ambaye ameshiriki filamu kama ‘Heart of fighter’ na ‘The Maid,’ kati ya zingine.
Pia Mkenya, Lupita Nyong’o  anayefanya kweli katika filamu za Hollywood anayeshiriki filamu kama Black Panther na 12 Years a Slave. Anaponda wananchi wengi ambao hupuuza pia hukosoa kazi za wasanii wazalendo.
”Hali hiyo ndio hufanya wengi kuzipa kisongo kazi za wazalendo na kuvutiwa na filamu za wasanii wa kigeni kama Afrika Kusini na Nigeria kati ya mataifa mengine,” akasema.  Anashauri wenzie wawe makini kwa kile wanachohitaji wanapojiunga na tasnia ya uigizaji.
”Kama ilivyo katika sekta zingine jukwaa la maigizo kamwe hali sio mteremko limejaa pandashuka nyingi tu ambapo ni rahisi kwa msanii kupoteza mwelekeo endapo atasahau azma yake,” akasema.
Anasema kuwa uigizaji unahitaji uvumilivu maana mafanikio kamwe hayapatikani rahisi. Anadokeza kuwa ingekuwa vizuri kama serikali inaweza kutega fedha kusaidia sekta ya uigizaji maana wapo wasanii wengi tu humu nchini ambao hawajapata nafasi kuonyesha vipaji vyao.
Anatoa wito kwa wenzake waliotangulia wakome kuwapigia chini waigizaji wanaokuja kwenye gemu.
  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Kenya isikubali kutishwa na Somalia

Irene analenga kufikia Sho Madjozi kimuziki

T L