• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Kenya isikubali kutishwa na Somalia

DOUGLAS MUTUA: Kenya isikubali kutishwa na Somalia

Na DOUGLAS MUTUA

IJAPOKUWA naishi nchi ya watu, daima mambo mawili hunikumbusha kuwa mimi ni Mkenya mzalendo: Michezo ya riadha na ugomvi kati ya Kenya na majirani zake.

Wanariadha wetu wanaposhiriki mashindano kokote duniani mimi huwa silali, sikwambii kamwe siketi wakikimbia hata mbio ndefu za marathon.

Wakishiriki mbio fupi – mathalan mita 100 ambazo nyota Ferdinand Omanyala ametokea kutamba kwazo – binafsi huhema kama wao ilhali mimi huzitazama kwenye runinga tu.

Juzi Waganda wenye majina yanayotamkika Kikenya walipoanza kushinda mbio za kimataifa niliwaza iwapo uraia wao unapaswa kuchunguzwa.

Hata hivyo, najua tuna historia ndefu ya ujirani na Uganda eneo la magharibi, hivyo tafakuri zangu hizo hazikutamba mbali.

Lakini zilinikumbusha enzi ya mwanzilishi wa taifa, Mzee Jomo Kenyatta, wakati ambapo kachinja wa Uganda, Iddi Amin Dada alidai mpaka wetu na Uganda uko Naivasha.

Wazalendo waliandaa maandamano na kutishia kuvamia Uganda ili kumtia adabu nduli yule na, kama kawaida ya nduli akitishiwa, alitukoma.

Nakumbuka nikiudhika hadi ya kuudhika pale mzozo kati ya Kenya na Uganda kuhusu kisiwa cha Migingo ulipotokota.

Nililiandikia kwa fujo suala hilo, nikakumbusha wasomaji kwamba waanzilishi wa taifa letu walilimwagia damu na hawangeruhusu hata inchi moja itwaliwe na taifa jingine.

Niliudhika zaidi na kauli ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwamba kisiwa chenyewe kiko Kenya, lakini maji yako Uganda.

Mantiki yake ilikuwa kwamba samaki wengi tu waliomo majini ni mali ya Uganda, Wakenya tukitaka tuchukue mwamba usio na manufaa makubwa kwetu ati.

Alipandisha na bendera ya Uganda kisiwani huko. Kufumba na kufumbua, polisi wa Uganda walianza kuwakamata wavuvi wetu, kuwatesa na kuwazuilia kwa muda mrefu.

Nilichemka zaidi Serikali ya Kenya ilipokosa kumjibu dikteta huyo, ikasema tu Uganda ni mshirika wetu mkuu wa biashara eneo hili, nikaona tumedharauliwa kweli! Nchi haili diplomasia ikashiba!

Badala ya Kenya kulishinikiza taifa hilo linalotegemea bandari yetu kuingiza mizigo kutoka nje liachie kisiwa chetu, ilianza kujipendekeza kwa Museveni.

Nilitabiri huo ndio uliokuwa mwanzo wa Kenya kusumbuliwa na majirani zake kama vile Tanzania, Ethiopia na Sudan Kusini. Hakika sasa hatuishi misukosuko mipakani.

Naungama sikudhani uhasama kati yetu na Somalia ungetokea Bahari Hindi! Nilijua magaidi wa Al-Shabaab wanasumbua mara kwa mara, lakini wangedhibitiwa.

La ziada ni kuwa nilidhani mipaka yetu iko salama kabisa baharini kwa kuwa hata jeshi letu la majini liko imara zaidi eneo hili la Afrika Mashariki.

Kama mpenzi wa masuala ya kijeshi, mara kwa mara mimi hufanya tafiti kuhusu uwezo wa kivita yalionao mataifa ya eneo hili na dunia kwa jumla.

Hakuna jeshi lililo na silaha hatari na za kisasa kuliko Kenya katika kanda ya Maziwa Makuu. Vita vikizuka, baharini tuko imara.

Lakini sasa nguvu hizo zimetishiwa pakubwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ambayo imetupokonya zaidi ya nusu ya milki yetu baharini ikaipa Somalia.

Hii ina maana hatuwezi kuendelea kujilinda kama mwanzo, hatuwezi kupanua jeshi letu la majini kwa idadi ya wanajeshi wala silaha na meli tutakavyo.

Hili ni suala la usalama wa kitaifa; lazima lichukuliwe kwa mazingatio yanayofaa, lau sivyo Kenya iwe kifaa cha kuchezewa na kila jirani aliye na muda wa kupoteza.

Mahakama hiyo imepuuza ilivyo mipaka ya mataifa mengine yaliyo na milki Bahari Hindi, ikainyanyasa Kenya kwa kushawishiwa na mataifa yanayoichochea Somalia ili yauziwe visiwa vyenye madini tele huko. Hatuwezi kukubali kunyanyaswa hivyo!

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) anapaswa kutoa amri ili KDF izuie yeyote kugusa sehemu yoyote tunayodai. Amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga.

[email protected]

You can share this post!

KDF yafichua ilivyoteka Kismayu na Al-Shabaab

Anita: Analenga kutesa katika uigizaji na masuala ya urembo

T L