• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Apewa talaka kwa kutotii dini, miraa ikichangia

Apewa talaka kwa kutotii dini, miraa ikichangia

Na STEPHEN ODUOR

MWANAMKE mmoja katika eneo la Bura, Kaunti ya Tana River ameomba talaka kutoka kwa mumewe akidai kuwa jamaa huyo hakuwa mwaminifu kwa imani ya Kiislamu.

Bi Asma, alimripoti mumewe Ahmed kwa wazazi baada ya kumpata kwa rafiki zake akitafuna miraa saa nane mchana wakati alipaswa kufunga.

Baadaye Bi Asma aliripoti suala hilo kwa Ustadhi wa eneo hilo, na kumtaka aanzishe hatua za talaka kutoka kwa mume huyo aliyedai kuwa ni mwongo.

“Mwanaume ambaye hawezi kuwa mwaminifu katika mambo ya dini hasa Ramadhan hawezi kuwa mwaminifu katika ndoa, ni mwanaume asiye na nidhamu na hatasaidia kulea watoto ipasavyo,” aliteta.

Kulingana na Bi Asma, mume huyo huondoka nyumbani kila mara baada ya swala ya adhuhuri ili kuungana na marafiki zake mjini tangu Ramadhani kuanza, akirudi tu jioni na futari.

Hata hivyo, Bi Asma anasema kuwa aliingiwa na shauku baada ya baadhi ya ndugu zake kumweleza kuwa mume huyo haendi msikitini kama inavyotakiwa na angeonekana tu akitoka kwenye nyumba za kupanga na vijana wenye tabia za kutiliwa shaka.

Hapo ndipo alipomfuata mumewe mahali hapo na kumkuta yeye na marafiki zake wakitafuna mirungi na kuizamisha na chupa baridi ya soda.

“Nilimkubali kwa sababu wazazi wangu waliamini kuwa ni mtu wa kanuni, lakini amethibitisha mapema sana, tuna wiki sita tu kwenye ndoa hii, na kinachofuata atakuja na mke wa pili nikiwa na ujauzito wangu wa mtoto wa kwanza, siwezi kumwamini,” alisema.

Mwanamke huyo amerejea nyumbani kwa wazazi wake akisubiri suala hilo kushughulikiwa.

Bw Ahmed kwa upande mwingine ameelezea majuto yake, akibainisha kuwa matendo yake hayakuwa ya makusudi bali yalitokana na hali yake ya kiafya.

“Nina vidonda vya tumbo na ninapokaa kwa muda mrefu bila chakula nasikia maumivu makali, hivyo natumia miraa kupunguza makali ndiyo maana naweza kufunga kwa nusu siku tu,” alisema katika mahojiano kwa njia ya simu.

Mwanamume huyo anabainisha kwamba hayuko tayari kwa talaka na atatimiza ahadi nyingine zote, akimsihi mke wake azingatie mazungumzo na wala sio talaka.

Wazee wa familia hizo mbili wameanza mazungumzo ili kusuluhisha suala hilo, huku ustadhi wa eneo hilo akibainisha kuwa talaka itakuwa suluhu la mwisho.

“Tunaweza kupanga mwanaume afunge siku kumi zijazo baada ya Eid ili kufidia uhuni hata ikibidi tumfungie chumbani na kumlisha mara moja kwa siku, aliweka ahadi kwa mkewe na ana jukumu la kulitimiza,” akasema Mahmoud Mohammed, kiongozi wa dini.

 

  • Tags

You can share this post!

Waislamu kuadhimisha Eid al-Fitr kesho Ijumaa

Madereva 2 watozwa faini jumla Sh170, 000 kwa kusababisha...

T L