• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Atwoli sasa agutuka kuhusu gharama ya maisha

Atwoli sasa agutuka kuhusu gharama ya maisha

NA WINNIE ATIENO

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli, sasa amelalamikia hali ngumu ya maisha inayowakumba Wakenya akimtaka Rais William Ruto kuokoa wafanyakazi.

Msimamo huu wa Bw Atwoli umetokea wiki chache baada ya kukosolewa na baadhi ya viongozi akiwemo kinara wa Azimio, Bw Raila Odinga, kwa madai kuwa ameungana na serikali akasahau kutetea maslahi ya wananchi.

Akiongea jana kwenye mkutano wa kamati ya vyama vya wafanyakazi duniani mjini Mombasa, Bw Atwoli alilaumu kuongezwa kwa bei ya mafuta kusababisha hali hiyo ngumu ya maisha na kupanda kwa uchumi.

Bw Atwoli alisema kampuni nyingi zimeongeza bei za bidhaa huku kukiwa hakuna nyongeza yoyote ya mishahara kwa wafanyakazi.
Kulingana naye, serikali inafaa kuandaa mashauriano na COTU kuhusu changamoto zinazokumba wafanyakazi ili kupatikane suluhisho ya kuleta afueni kwa raia.

“Hii ndio shida inayotukumba katika nchi hii. Ukiongeza bei ya mafuta bei ya kila kitu kingine hupanda. Ndio maana tunataka kukutana na Rais Ruto na asasi nyingine serikalini ili tujadili kuhusu uchumi. Uchumi umesambaratika vibaya sana,” akasema Bw Atwoli.

Kulingana naye, serikali na waajiri wengine nchini wanafaa kuzingatia kuwaongezea wafanyakazi misharaha ili waweze kukabiliana na changamoto za hali ngumu ya maisha.

Bw Atwoli alionya kuwa, COTU haitaki kupeleka wafanyakazi barabarani kuandamana kabla ya kujaribu mazungumzo.

“Lakini sababu serikali imekuwa mamlakani kwa mwaka mmoja pekee, tumewaambia kupitia barua kwamba ipo haja ya kufanya kikao na Rais Ruto, Wizara ya Fedha ile ya Leba na bodi ya COTU kujadili endapo Kenya inaelekea mkondo mzuri ama mbaya,” aliongeza.

Alisema huenda ikawa wataalamu wa uchumi wa serikali hawajui masaibu ambayo Wakenya wanapitia.

“Pengine hata hao wadadisi wa uchumi hawajui mambo yanayoibuka ikilinganishwa na yale ambao wanauchumi wa wafanyakazi wanafahamu. Ndio maana tunasema lazima tubadilishane mawazo ili tuokoe maisha,” aliongeza.

Alieleza kuwa, si haki kwa gharama ya maisha kuzidi kupanda huku pia ushuru ukipanda ilhali mishahara ya wafanyakazi haibadiliki.

Mwezi uliopita, Bw Atwoli alikashifiwa na viongozi mbalimbali kwa msimamo wake wa kuunga mkono hatua ya serikali kutoza ushuru wa nyumba wa asilimia tatu kwa waajiriwa.

“Tunataka wakiongeza bei za vitu ambavyo wanataka kuongeza au hata ushuru, lazima ziambatane na nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi,” akasema.

Alisihi yyama vya wafanyikazi Barani Afrika kuendelea kushirikiana, kujiongoza kijeshi ili kupigania haki za wananchiakionya kuwa endapo watalegeza kamba hakuna serikali wala mwajiri watakuwa wakiandikishana nao ili kuongeza mishahara ya wafanyakazi.

Bw Atwoli alisema COTU itaendelea kuishauri serikali kuhusu uchumi hadi pale uchumi utakapoimarika tena, wafanyikazi wanalipwa vizuri na kulindwa.

“Wakienda mrama pia tutawaarifu na kuwaonyesha njia bora ya kufuata na tunajua lazima watafuata maagizo yetu sababu hawana budi,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

DONDOO: Jombi achanganywa na demu mgeni plotini aliyemwomba...

Wafanyabiashara waliofurushwa kimadharau CBD walipwa...

T L