• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Azimio waendelea kumlima Gavana wa Turkana kufuatia kufurushwa kwa Raila katika hafla

Azimio waendelea kumlima Gavana wa Turkana kufuatia kufurushwa kwa Raila katika hafla

NA LABAAN SHABAAN

KIONGOZI wa Chama Cha Wiper Kalonzo Musyoka na wa Narc Kenya Martha Karua wamezidi kukeketwa maini na tukio la Kiongozi wao Raila Odinga kuzuiwa kuhutubia umati katika Kaunti ya Turkana mnamo Oktoba 13, 2023.

Kinara wa Wiper amemrushia cheche Gavana wa kaunti hiyo Jeremiah Lomurkai ambaye amejenga ukuruba na Rais William Ruto.

Kulingana Bw Kalonzo, gavana huyo ameshirikiana na rais ili ajiondolee kesi ya ‘kukosa vyeti hitajika vya elimu’ ili kuwa gavana.

Akizungumza walipohudhuria ibada ya maombi Kaunti ya Kajiado, Bw Kalonzo alimsifu Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku kwa kusimama na Muungano wa Azimio.

“Gavana Lenku angekuwa kama mwenzake wa Turkana lakini ameonyesha msimamo,” alisema Bw Kalonzo akiashiria Bw Lomurkai ametishwa na serikali kuwa atafunguliwa mashtaka.

“Gavana wa Kajiado hawezi kuleta aibu kwa Bw Odinga. Kwa sababu hana ‘makaratasi’ anaona Kenya Kwanza itamwandama. Tutakutetea sisi ni mawakili,” aliongeza.

Bw Kalonzo alikuwa anarejelea tukio la Kiongozi wa Azimio kuzuiwa kuhutubia hadhira katika Tamasha ya Utamaduni wa Kiturkana (Tobong’u Lore) Kaunti ya Turkana.

Katika sherehe hizo, baadhi ya viongozi wa kaunti walilalamikia chama cha ODM wakidai maslahi ya jamii yamepuuzwa licha yao kuunga mkono chama.

Fujo zilizuka baada ya wafuasi waliotaka Bw Odinga kuhutubu kukabiliana na kundi jingine.

Vurumai hizi zilizuia kufanyika kwa hotuba za viongozi wa Azimio.

Bi Karua alisema viongozi wa Turkana walimkosea heshima Bw Odinga baada ya kutumwa na upande wa serikali.

“Kitendo kilichofanyika kule Turkana kilikuwa ni cha aibu. Huwezi kupatiwa kipazasauti ukiwa MCA uanze kumtupia maneno kiongozi kama Raila Odinga, Siwezi kumlaumu huyo mama: kuna mtu alimtuma kufanya kazi fulani,” alisema Bi Karua akirejelea shutuma kwa Bw Odinga zilizotoka kwa Diwani wa Lodwar Mjini, Ruth Kuya.

Gavana Lomurkai anakabiliwa na kesi ya kughushi shahada na stashahada zinazodaiwa kutolewa na Chuo Kikuu cha Methodist.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mwanamume aliyebakwa anaweza kulinda ushahidi

Jamii ya Wanandi yaitaka Uingereza kuilipa fidia ya Sh20...

T L