• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Jamii ya Wanandi yaitaka Uingereza kuilipa fidia ya Sh20 bilioni kutokana na mateso ya kikoloni

Jamii ya Wanandi yaitaka Uingereza kuilipa fidia ya Sh20 bilioni kutokana na mateso ya kikoloni

STANLEY KIMUGE NA BARNABAS BII

IKIBAKI wiki moja kabla ya Mfalme Charles III wa Uingereza kuzuru nchini Kenya, wazee wa jamii ya Nandi wanatoa shinikizo kwa taifa hilo kuilipa fidia ya Sh20 bilioni, kurejesha fuvu la shujaa Koitalel Samoei na vito vilivyoibwa wakati wa ukoloni.

Haya yalisemwa na wazee na viongozi wa kisiasa wakati wa makala ya 118 ya ukumbusho wa shujaa huyo wa jamii ya Nandi, sehemu liliko kaburi la Koitalel, eneobunge la Nandi Hills.

Inaaminika fuvu hilo la Koitalel liko katika Makavazi ya Pitts Rivers jijini London, Uingereza.

Jamii ya Nandi kupitia kwa wazee na viongozi wake, inataka fidia ya Sh20 bilioni kutoka kwa serikali ya Uingereza kwa hasara iliyotokea wenyeji walipofukuzwa kutoka kwa ardhi yao ya tangu jadi, mauaji ya shujaa Koitalel na wengine alioshirikiana nao kuipa jamii mwelekeo, miongoni wa dhuluma nyingine dhidi ya binadamu zilizotekelezwa na wakoloni.

Shinikizo hizi zinajiri wakati maandalizi ya ziara hiyo ya kipekee yamepamba moto.  Itakuwa mara ya kwanza kwa Mfalme Charles III na mkewe, Malkia Camilla, kwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Madola tangu alipotawazwa Septemba 2023.

Ziara hiyo imeratibiwa kuanza Oktoba 31 hadi Novemba 3, 2023.

Taarifa kutoka kwa Kasri la Buckingham iliweka wazi ziara hiyo, baada ya Rais William Ruto kuwapa mwaliko “kusherehekea uhusiano na uhusiano mwema baina ya Kenya na Uingereza.”

Hata hivyo, jamii ya Nandi ingali inalia kwamba haijatendewa haki kwa muda huo wote, licha ya kuitisha fidia ya pesa na pia kurudishiwa fuvu la kichwa cha shujaa wao.

Rais Ruto amewahi kunukuliwa akisema kwamba amejitolea kuhakikisha suala la unyakuzi wa mashamba uliofanywa na wakoloni dhidi ya watu wa ukoo wa Talai na jamii ya Nandi, linashughulikiwa.

Koitalel, aliyekuwa kiongozi wa kisiasa na kitamaduni, aliiongoza jamii ya wazee 24 hadi alipouawa mnamo Oktoba 19, 1905.  Kifo hicho kilitokea baada ya mwanajeshi wa Uingereza, Kanali Richard Meinertzehagen, kumhadaa Koitalel na wazee wengine kwamba wangesitisha uhasama katika eneo la Ket Barak, ambako sasa ni makao ya Nandi Bears Club.

Viongozi wa Nandi, wakiongozwa na mbunge wa Emurua Dikirr Johanna Ng’eno na Naibu Gavana wa Nandi Yulita Cheruiyot, walisema ipo haja ya fuvu la kiongozi huyo kurejeshwa ili familia yake impe mazishi ya heshima.

“Familia inataka kumzika Mzee na pia watu wengi waliuawa bila familia zao kupewa fidia,” akasema Bw Ng’eno.

Mtaalamu katika makavazi ya Koitalel Samoei, Bw Francis Talam, mawakili wakiongozwa na Kimaiyo Sego, wanakusanya ushahidi kuhusu vifaa vilivyoibiwa.

“Wataalamu na viongozi wanashinikiza ni lazima fidia ilipwe,” akasema Bw Talam.

Mchakato mwingine wa fidia ulikuwa umeanzishwa na aliyekuwa gavana wa Nandi, Cleophas Lagat, ambapo Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Karim Khan na kampuni ya mawakili ya Lilan & Koech, walitwikwa jukumu la kukusanya ushahidi kuwasilisha  ICC kuhusu jinsi watu walivyofurushwa kutoka makazi yao na hatimaye Koitalel Samoei akauawa.

  • Tags

You can share this post!

Azimio waendelea kumlima Gavana wa Turkana kufuatia...

Vyama 38 vipya mbioni kusajiliwa kupigania mabilioni kutoka...

T L