• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Baada ya kufukuza World Coin, Wakenya kutambuliwa kwa kumulikwa mboni ya jicho

Baada ya kufukuza World Coin, Wakenya kutambuliwa kwa kumulikwa mboni ya jicho

Na CECIL ODONGO

Miezi miwili baada ya serikali kufukuza kampuni ya sarafu ya mitandaoni World Coin kwa kutumia mitambo ya kumulika mboni ya jicho kuwasajili Wakenya, serikali sasa inasema raia watatambuliwa kwa njia hiyo badala ya kubeba kitambulisho.

Rais William Ruto jana alisema Wakenya watakuwa wakitambuliwa kupitia mboni ya  jicho lao kumulikwa au kupitia alama za vidole wakisaka huduma za serikali.

Watakuwa wakitambuliwa hivyo badala ya mtindo wa tangu zamani ambao ulizoeleka ambapo lazima Mkenya aonyeshe kitambulisho kabla ya kuhudumiwa kwenye afisi za serikali.

“Tayari kitambulisho cha kidijitali ambacho kimekuwa tatizo kwetu kwa sasa kinafanyiwa majaribio katika kipindi cha miezi miwili kinachokuja,” akasema Rais Ruto.

“Nimehakikishiwa na washikadau wote ikiwemo wizara husika kuwa mnamo Disemba tutazindua kitambulisho cha kidijitali,” akaongeza Rais Ruto.

Rais alikuwa akizungumza Mavoko, Kaunti ya Machakos Jumatatu, Oktoba 30, 2023 wakati wa uzunduzi wa vifaa vya kiteknolojia vilivyotengeneza nchini.

“Mkenya hatajitajika kubeba kitambulisho ila watatambuliwa kidijitali kwa kumulikwa mboni ya jicho au kupitia kuchukuliwa alama za vidole. Hii itawasaidia kuendelea na shughuli zao bila tatizo la kutambulishwa,” akasema.

Kampuni hiyo ya sarafu ya mtandaoni inayotumia teknolojia ya ‘blockchain’ ilipigwa marufuku nchini mnamo Agosti, serikali ikidai ilikuwa inalenga kutumia vibaya data za Wakenya.

Maelfu ya Wakenya walikuwa wamejitokeza Jumba la KICC ambapo World Coin ilikuwa ikichukua data zao kupitia kuwamulika mboni ya jicho kisha kuwalipa Sh7,000.

Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki alikuwa amesema kuwa World Coin haikuwa imeeleza jinsi ambavyo ingetumia data ya Wakenya.

“Vitengo vya usalama, mashirika ya kifedha na mamlaka ya kuhifadhi data za Wakenya wameanzisha uchunguzi kubaini uhalali na uzingativu wa sheria kwenye shughuli inayoendeshwa na kundi hilo na usalama wa data zinazokusanywa pamoja na jinsi zitahifadhiwa ziwe salama,” alisema Bw Kindiki mnamo Agosti 2.

Wakati World Coin ilipokuwa ikiendeleza shughuli hiyo, Wakenya wengi waliojitokeza walikuwa wakisema kuwa ukosefu wa ajira na umaskini ndio uliwasukuma waendee Sh7,000 ambazo zilikuwa zikitolewa na World Coin.

  • Tags

You can share this post!

Tambua kwa nini ‘kabeji za kichina’ ndio mpango mzima...

Jinsi wanafunzi Homa Bay walivyovamia mwalimu mkuu...

T L