• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Tambua kwa nini ‘kabeji za kichina’ ndio mpango mzima kwa walio na kiu ya kutafuta pesa

Tambua kwa nini ‘kabeji za kichina’ ndio mpango mzima kwa walio na kiu ya kutafuta pesa

NA RICHARD MAOSI

‘Kabeji za Kichina’ almaarufu pakchoy zinazidi kupata umaarufu humu nchini kutokana na manufaa yake mengi kiafya.

Ladha yake  ni nzuri na matawi yake huwanda pale zinapokomaa, hii ikimaanisha mkulima anaweza kupata mavuno mazuri mwisho wa msimu, endapo atafuata utaratibu wa kuzikuza.

Asilimia 95 ya pakchoy huwa ni maji, asilimia 2 ikiwa wanga kwa maana ya starch, asilimia moja protini na chini ya asilimia 3 ni mafuta.

Akilimali ilizuru kijiji cha Kimuyu, Kaunti ya Kiambu ambapo tunakumbana na mkulima Jane Kimari ambaye anatumia mfumo wa kisasa wa mashamba ya ghorofa (storey garden) kukuza mboga.

Kimari anasema kwa sababu ya uhaba wa mashamba katika sehemu nyingi za Mkoa wa Kati, aliamua kutumia teknolojia hii ili kuhakikisha kuwa anakuza chakula kwa matumizi ya nyumbani na vilevile kuuza sokoni.

Kulingana na Kimari, pakchoy ni spishi ya mboga ambazo zinaweza kukuzwa shambani kwenye mikebe au konteina maalum ikiwa ni pamoja na kukuzwa kwenye mchanga ambao umechanganywa vyema na mbolea asilia ambazo husaidia kuhifadhi unyevu.

Alijifunza kukuza pakchoy alipozuru mojawapo ya Maonyesho ya Kilimo Kaunti ya Kiambu, ambapo alipata maarifa namna ya kupanda, kutunza, kuvuna na kutafutia soko mazao yake.

Anasema maandalizi ya mapema huanza kwa kuondoa magugu, ili kutoa nafasi nzuri ya mizizi kupenya ardhini kwa ajili ya kutafuta virutubishi.

Jane Kimari kutoka kijiji cha Kimunyu Kaunti ya Kiambu akikagua shamba lake la mboga za Kichina za pakchoy. PICHA|RICHARD MAOSI

Kinyume na mboga za kawaida mboga za pakchoy huuzwa sokoni kati ya Sh130-150 kwa kilo.

Kimari anakuza aina mbalimbali ya matunda zikiwemo strawberries, nyanya, sukumawiki, kabeji na spinach lakini alianza kukuza pakchoy baada ya kupata kundi maalum la wanunuzi.

Pili alitaka kupunguza ushindani mkali baina ya wakulima kutoka kijijini kuwa wengi wao bado wanakuza mboga za kiasili ambazo huwa zimezoeleka.

Anasema pakchoy hupikwa kama kabeji au sukumawiki na huchukua kati ya dakika tatu hadi tano kuiva.

Vilevile mboga hizi zinaweza kuliwa zikiwa ghafi na ndio maana mara nyingi hushauriwa kutumika kwenye viungo vya lishe kama saladi.

Alifichulia Taifa Leo kuwa mboga za pakchoy zinaweza kukaushwa kisha zikahifadhiwa kwa muda mrefu kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Ni aina ya mboga ambazo huwa zimebeba  madini ya patassium, calcium, phosphorus na vitamini hivyo basi hulenga kuwasaidia wenye matatizo ya moyo, kusafisha damu na kuimarisha mzunguko wa hewa safi mwilini.

Anasema utaratibu wa kukuza mboga za pakchoy huwa ni mwepesi almuradi mkulima atakuwa amezipata mbegu sahihi kutoka kwenye taasisi zinazofahamika kuuza mbegu.

Mkulima anatakiwa kupanda mazao yake kwa namna ya kipekee ili kuhakikisha matawi yanafikiwa na miale ya jua angalau kwa asilimia 50 ili kutengeneza rangi ya kijani kibichi iliyokolea.

Pakchoy hufanya vyema kwenye kiwango cha kadri cha jua. Zinafaa kupigwa na miale ya jua kati ya masaa matatu hadi nne kila siku,” akasema, huku akiongezea kuwa hukuzwa kwenye maeneo ambayo hushuhudia kiwango kikubwa cha mvua.

Aidha, mkulima anashauriwa kukuza kiwango kidogo kidogo cha pakchoy, kwenye maeneo tofauti ya shamba lake ambayo atakua ameteua.

Hii ni kwa sababu mavuno yake huwa tayari katika kipindi cha wiki nne tu na atakua akiyavuna mazao yake kila mara.

  • Tags

You can share this post!

Mwanaume niliyemkataa amenitusi eti nina kisima...

Baada ya kufukuza World Coin, Wakenya kutambuliwa kwa...

T L