• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Baba na watoto washtakiwa kwa wizi wa Sh.54Milioni

Baba na watoto washtakiwa kwa wizi wa Sh.54Milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZi wa kampuni ya fedha alishtakiwa Ijumaa pamoja na watoto wake wawili wa familia yake kwa wizi wa Sh54milioni.

Na wakati huo huo hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Francis Andayi alifahamishwa mkurugenzi huyo Bw James Ndwiga Muchungu amemzuia  muwekezaji katika kampuni ya Meridian Acceptance Limited (MAL) kuingia katika afisi za kampuni hiyo.

Bw Andayi aliombwa asiwaachilie Muchungu , Ian Nyaga Ndwiga na Lisa Mumbi Ndwiga kwa vile muwekezaji huyo Bw Eduardo Hernadez De La Rosa Ciriza pamoja na watu wa familia yake wametishiwa maisha.

Bw Andayi alielezwa kuwa nduguye Eduardo,  Bw  Gonzalo Hernadez Ciriza alikufa katika mazingira yasiyoeleweka alipokorofishana na Bw Muchungu wakiwa kazini.

Wakili Mwendwa Mwinzi anayewakilisha Eduardo alimweleza Bw Andayi kwamba Gonzalo alizirai na kufariki akiwa ndani ya gari lake karibu na kituo cha polisi cha Central muda mfupi baada ya kuvurugana na Bw Muchungu wakiwa afisini.

Eduardo Hernadez De La Rosa Ciriza, mlalamishi katika kesi waliyoshtakiwa watu hao wa familia moja…Picha/RICHARD MUNGUTI

“Nduguye Eduardo alipokea vitisho kutoka kwa Bw Muchungu wakiwa afisini. Wafanyakazi wengine walishuhudia vurugu hiyo. Gonzalo aliaga baada ya muda usio mrefu ndani ya gari lake karibu na kituo cha polisi cha Central,” Bw Mwinzi alimweleza Bw Andayi.

Wakili huyo aliyewasilisha afidaviti ya kupinga washtakiwa hao kwa dhamana alieleza korti mlalamishi (Eduardo) ambaye ni raia wa Uhispania anahofia maisha yake baada ya kufariki kwa nduguye.Hakimu alifahamishwa bw Muchungu alibadilisha kufuli katika afisi za kampuni hiyo ya MAL na amemkataza kabisa akiingia afisini.

Mahakama ilielezwa Eduardo ameekeza zaidi ya Sh380milioni katika kampuni hiyo ya MAL ambapo Bw Muchungu aliwatimua kazi wafanyakazi wengine na kuwaajiri watu wa familia yake.Bw Mwinzi alieleza mahakama kuwa mnamo Desemba 2020 bodi ya MAL ilimtimua kazini Bw Muchungu na hivyo basi yuko afisi kimakosa.

Lakini mawakili Charles Njenga na Brian Mureithi Muchiri wanaowakilisha  Bw Muchungu , Bw Ndwiga na Bi Ndwiga alieleza mahakama vurugu katika kampuni hiyo inatokana na usimamizi wake.“Kesi hii inatokana na usimamizi wa kampuni hii kama mashtaka dhidi ya watatu hawa yanavyodai,” Bw Njenga.

Bw Njenga alisema kuna kesi tatu katika mahakama kuu kuhusu uongozi wa kampuni hii ya MAL.“Hata leo Jaji David Majanja alitoa uamuzi katika kesi mbili zilizoshtakiwa na Eduardo.Alitupilia mbali ombi Eduardo atambuliwe kuwa mmiliki na msimamizi wa MAL,” Bw Njenga alimweleza hakimu.

Watatu hao wameshtakiwa kwa kula njama za kuibia MAL Sh176.9milioni kati ya Januari 1 2017 na Desemba 31 2020.Muchungu ameshtakiwa kuibia MAL Sh23milioni ilhali Ian amekabiliwa na shtaka la wizi wa Sh20milioni naye Lisa amekana kuiba Sh10milioni mali ya MAL.

Bw Andayi aliamuru washtakiwa wazuiliwe hadi Agosti 16, 2021 atakapotoa uamuzi wa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

Messi kusubiri zaidi kuchezea PSG baada ya kutambulishwa...

Yaya afungwa miaka miwili kwa kuiba mikufu