• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Bandari: Wachukuzi watoa masharti kwa serikali

Bandari: Wachukuzi watoa masharti kwa serikali

Na KALUME KAZUNGU

MUUNGANO wa wamiliki wa kampuni za uchukuzi nchini (KTA), imetoa masharti yanayofaa kutimizwa na serikali kwanza kabla ya kuanza shughuli za kusafirisha mizigo kutoka bandari mpya ya Lamu hadi sehemu nyingine za nchi na mataifa jirani.

Serikali ilitangaza kufunguliwa rasmi kwa bandari ya Lamu ifikapo Mei 30 ilhali meli ya kwanza ya mizigo ikitarajiwa kutia nanga kwa mara ya kwanza katika historia bandarini humo kufikia Mei 20 mwaka huu.

Akizungumza wakati alipoandamana na wadau mbalimbali kuzuru bandari ya Lamu kutathmini maendeleo eneo hilo, Afisa Mtendaji wa KTA nchini, Bw Dennis Ombok, alisema ipo haja ya serikali kuimarisha usalama kwenye barabara mbalimbali za Lamu, Tana River, Garissa na sehemu zingine za kaskazini mwa Kenya wakati bandari hiyo itakapofunguliwa mwezi huu.

Barabara za Lamu, ikiwemo ile ya Lamu-Witu-Garsen, Lamu-Tana River-Garissa-Nairobi na nyinginezo zilizoko kaskazini mwa Kenya, kwa miaka mingi zimeshuhudia mashambulizi ya Al-Shabaab, ambapo madereva wa magari ya uchukuzi, abiria wa mabasi ya usafiri wa umma, wale wa magari ya kibinafsi na hata walinda usalama wakiishia kufariki au kujeruhiwa.

Bw Ombok alisema ili kuwaruhusu madereva wa malori na matrela kuanza kazi ya uchukuzi kutoka bandari ya Lamu, lazima serikali iwahakikishie usalama wao.

Bw Ombok pia aliiomba serikali kupunguza bei ya mafuta, ikiwemo petroli na dizeli hasa kwa madereva wa malori na matrela zitakazokuwa zikisafirisha mizigo kutoka bandari ya Lamu hadi maeneo mengine nchini na kimataifa.

Alitaja suala la kodi inayotozwa kontena na mizigo mingine pia kupunguzwa ili kuwapa moyo wachukuzi kuendeleza kazi zao kwenye bandari hiyo mpya.

Pia aliiomba serikali kupunguza bei ya vipuri vya magari, ikiwemo magurudumu na vifaa vingine hasa kwa wamiliki wa magari hayo ya uchukuzi watakaokuwa wakihudumu kwenye barabara za Lamu.Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alisema serikali imefanya kila jitihada kuhakikisha Lamu iko na usalama wa kutosha.

Alisema maafisa wa polisi na jeshi (KDF) wamesambazwa kila mahali, barabarani, vichochoroni, msituni, angani na baharini katika harakati za kudhibiti usalama eneo hilo.Aliwataka wadau wote kuondoa hofu kwani usalama wao umelindwa vilivyo.

“Kama serikali, tuko tayari kwa ufunguzi wa bandari ya Lamu. Amani imedumishwa. Usalama umedhibitiwa. Hakuna la kuhofia,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

Madiwani 78 wakataa mwaliko wa kukutana na Moi

MARY WANGARI: Wazazi watumie likizo kuwapa watoto malezi...