• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Baraza la viongozi wa kidini kuhusu Covid-19 laongezewa miezi sita zaidi

Baraza la viongozi wa kidini kuhusu Covid-19 laongezewa miezi sita zaidi

Na SAMMY WAWERU

BARAZA la Mashirika ya Kidini limeongezewa muda zaidi ili kuendelea kuangazia mikakati inayopaswa kufuatwa kwenye maeneo ya kuabudu kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, alitangaza Ijumaa kwamba baraza hilo limeongezewa miezi sita zaidi.

Maeneo ya kuabudu yalipofungwa Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa Covid-19 Machi 2020, bazara hilo linaloongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Nyeri, Kanisa la Katoliki, Antony Muheria lilibuniwa ili kutoa mwelekeo na hasa utaratibu wa kufunguliwa tena kwa maeneo hayo.

“Kipindi cha Baraza la Mashirika ya Kidini kilifikia kikomo mwaka wa 2020 ulipokamilika. Tunakiongezea muda zaidi, wa miezi sita kuanzia leo Januari 1, 2021, ili kiweze kutusaidia,” waziri akasema.

Baraza hilo limekuwa lenye mchango mkuu katika kuelekeza maeneo ya kuabudu, ikiwa ni pamoja na kutoa idadi ya wanaopaswa kuhudhuria ibada, muda wa kuendesha ibada, mpangilio wa viti na kutilia mkazo sheria na mikakati kuzuia kuenea kwa corona.

Bw Kagwe amewataka Wakenya kujua taifa hili halijashinda vita dhidi ya janga la corona, licha ya idadi ya maambukizi kuonekana kushuka.

Ijumaa, katika kipindi cha saa 24 visa vya maambuzi mapya vilikuwa 156 kutoka kwa sampuli 4,317 huku wagonjwa 11 wakiangamia.

You can share this post!

Pochettino kushawishi PSG kurefusha mikataba ya Neymar na...

Kibarua kigumu kwa wanavoliboli wa Kenya kimataifa baada ya...