• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Benki ya NCBA yazindua tawi la Ruiru

Benki ya NCBA yazindua tawi la Ruiru

Na LAWRENCE ONGARO

WAFANYABIASHARA wa kaunti ndogo ya Ruiru, Kaunti ya Kiambu watanufaika pakubwa na huduma za kifedha baada ya benki mpya ya NCBA.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na washika dau wengi wanaojishughulisha na biashara tofauti mjini humo na vitongoji vyake.

Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Bw John Gachora, alisema waliamua kufungua tawi Ruiru kutokana na ongezeko la wafanyabiashara mjini humo.

Alisema benki hiyo ina matawi mengine 76 kote nchini na tayari ilizindua tawi jingine hivi majuzi katika Kaunti ya Kakamega.

“Tutahakikisha ya kwamba tunatoa huduma ya kuridhisha kwa wateja wote watakaofungua akaunti zao kirahisi,” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema mji wa Ruiru unakua kwa kasi na kwa asilimia kubwa na kwa hivyo ni vyema kuwapa wafanyabiashara huduma inayostahili kutekeleza ili kuendeleza biashara zao.

“Tumekuja mjini Ruiru kwa sababu tunaamini ya kwamba mji huu una usalama wa kutosha na mazingira pia ni ya kuridhisha,” alisema Bw Gachora.

Bw Muhoho Kenyatta ambaye pia ni miongoni mwa wakurugenzi wakuu katika benki hiyo, alipongeza Kaunti ya Kiambu kwa kuwa mstari wa mbele kuipa nafasi benki hiyo kuwa hapo.

“Ninatumai ya kwamba biashara zilizo katika mji huu wa Ruiru na vitongoji vyake zitaimarika pakubwa,” alisema Bw Kenyatta.

Alisema ufanisi wa mfanyabiashara yeyote hutokana na yeye kuhakikisha anawekeza fedha zake katika benki.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro aliisifu benki hiyo ya NCBA kwa kufikiria kuwekeza katika mji huo.

“Tuna matumaini makubwa ya kwamba biashara nyingi zinazofanyika katika barabara kuu ya Bypass eneo la Kamakis zitanawiri zaidi na zitawekeza kwenye benki hii,” alisema gavana huyo.

Alisema mji wa Ruiru kwa sasa una idadi ya wakazi wapatao 400,000.

“Kutokana na idadi kubwa ya wakazi wa Ruiru, bila shaka benki hiyo itapata wateja wengi watakaoendesha biashara tofauti,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba wawekezaji wanakuja kwa wingi mjini Ruiru.

“Tunataka uchumi wa Kiambu uimarike kabisa. Kila mmoja ana nafasi sawa kuendesha biashara yake bila kuwekewa vikwazo,” alifafanua gavana huyo.

Alisema wakulima wa kiwango cha chini watapata nafasi pia kuendesha biashara zao bila kusumbuliwa.

“Nitafanya kongamano kubwa ili kualika washika dau wote wa kibiashara ili waeleze jinsi ambavyo wangetaka mwelekeo wa biashara ufanyike. Tunaona hiyo ndiyo njia pekee ya kuboreshe biashara katika eneo hili,” alisema gavana huyo.

You can share this post!

Nilimtusi Neymar, lakini si kwa ubaya – Mbappe

TSC yatuza shule, walimu waliofana zaidi masomoni