• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Biashara ya nyama inachangia mazingira kuzorota, kongamano laambiwa

Biashara ya nyama inachangia mazingira kuzorota, kongamano laambiwa

MARY WANGARI NA KNA

KUNDI la watetezi wa Haki za Wanyama Duniani limetoa wito kwa mataifa ya Afrika kuangazia maslahi ya mifugo katika mdahalo unaoendelea wa Kongamano la Mabadiliko la Tabianchi Afrika 2023.

Wakizungumza Jumatatu Septemba 4, 2023 jijini Nairobi, wanaharakati hao walihimiza kuanzishwa kwa mifumo mipya isiyo ya kikatili inayowezesha kustawisha sekta ya ufugaji.

Kwa mujibu wa watetezi hao kuhusu maslahi ya wanyama, kilimo cha viwanda hakijaangaziwa ipasavyo kama chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabia nchi licha ya kusababisha misitu kukatawa ili kupanda malisho ya mifugo ikiwemo uchafuzi wa hewa.

Kando na kuvuruga makazi asili ya wanyamapori, kilimo cha viwanda, wanaharakati wanasema, kinasababisha wanajamii kufurushwa na kujilimbikizia faida kutokana na ukatili unaotendewa mabilioni ya mifugo kila mwaka.

Wakiongozwa na Mkurugenzi wa Ulinzi wa Wanyama Duniani, Tennyson Williams, wamesisitiza kuwepo uhusiano kati ya kilimo kinachoegemea ufugaji na mabadiliko ya tabianchi wakisema mdahalo huu haupaswi kupuuzwa kamwe katika Kongamano.

Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi ambalo ni la kwanza kuwahi kufanyika Afrika lilianza rasmi Septemba 4, 2023 na linaendelea hadi kesho Septemba 6.

Ajenda kuu zilizopatiwa kipaumbele ni kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na gharama ya madhara hayo duniani na hususan katika nchi za Afrika.

“Juma hili, Afrika yote inakongamana Nairobi kutafuta suluhu kuhusu kero la tabianchi. Nia yetu ni kupigia debe mbinu bora za kilimo cha ufugaji, mifumo ya chakula cha kiasili Afrika na kupatia kipaumbele mashlahi ya wanajamii kutoka maeneo husika kama sehemu ya mbinu za ustawishaji zinazoweza kuhakikishia siku za usoni zilizo salama,” alisema Bw Williams.

Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Raslimali za Wanyama (AU-IBAR) Dkt Huyian Ahmed Salih alisema ukataji misitu kwa kiwango kikubwa, uharibifu wa mazingira, kuzidisha shughuli za kilimo kupita kiasi, mbinu hatari za ufugaji, biashara inayohusu aina mbalimbali za wanyama na mimea ndizo kiini cha mazingira kuzorota na kuzuka kwa magonjwa mapya.

Alitoa wito kuwepo mikakati thabiti inayounganisha maslahi ya wanyama, mazingira na maendeleo kijamii na kiuchumi huku akisisitiza haja ya kupatia kipau mbele maslahi ya wanyama katika Ajenda ya Mazingira na Ustawishaji Maendeleo Duniani.

“Imethibitishwa bayana kuwa mikakati kabambe ya ustawishaji, iliyoundwa kuwaangazia wakulima inaweza kuboresha mazao ya ufugaji na kugeuza mashamba na maeneo ya malisho kuwa vituo vya kuyeyusha kaboni, kukomesha ukataji misitu, kutumia mbolea zinazofaa na kuimarisha mikondo ya usambazaji bidhaa nchini na kimataifa,” alisema Mshauri kuhusu Usimamizi wa Maji na Mazingira katika Afisi ya Rais, Ismael Faheny.

Serikali za mataifa ya Afrika pamoja na Wajumbe wa TabiaNchi Afrika wamehimizwa kujumuisha katika Michango ya Kitaifa (NDCs) mikakati ya kukomesha hewa sumu inayotokana na ufugaji, mifumo ya chakula kwa wafugaji wadogo wadogo, kuimarisha mifumo ya chakula nchini na kimataifa na kutambua nafasi muhimu ya chakula cha kiasili Afrika.

  • Tags

You can share this post!

TUONGEE KIUME: Usichotakiwa kufanya ukiwa mwanamume usiye...

Wetang’ula atetea kusafirisha wafisadi mbinguni

T L