• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Biashara ya utumbo wa samaki aina ya Sangara yanoga Homa Bay

Biashara ya utumbo wa samaki aina ya Sangara yanoga Homa Bay

Na GEORGE ODIWUOR

Biashara ya utumbo wa sangara (Nile Perch) imevuma sana miongoni mwa wavuvi katika Ziwa Viktoria kuliko hata samaki wenyewe, kutokana na malipo mazuri yanayohusishwa nao.

Wavuvi wamekuwa wakiwauzia wanunuzi utumbo huo kwa bei ya juu zaidi na mvuvi anaweza kujizolea zaidi ya Sh35,000 kwa kila kilo. Utumbo kwa kawaida hutolewa ndani ya samaki wanaposafishwa ili kuzuia kuharibika kwao haraka.

Kutokana na kunoga kwa biashara hiyo, wavuvi wamekuwa wakiondoa utumbo huo kwa samaki hata kabla ya kuwafikisha ufuoni kutokana na jinsi ambavyo wateja wamekuwa wakiung’ang’ania ili kufaidika kifedha.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Fuo William Onditi, bei ya utumbo hutofautiana kutokana na ukubwa wake. Utumbo mkubwa humpa mvuvi pesa nyingi na inaaminika kuwa una soko bora hasa kule bara Asia.

Hata hivyo, wavuvi wengi bado hawajui jinsi utumbo huo unaofahamika kwa Kiluo kama ‘mondo’ unavyotumika baada ya kuuza. Bw Onditi alisema kuwa kuna dhana nyingi kuwa utumbo huo hutumika kutengeneza uzi wa kuwashonea wagonjwa hospitalini na wengine wakisema unatumika kutengeneza kifaa cha kukinga upepo kwenye ndege.

Biashara ya utumbo sasa imenoga sana katika fuo za Nyandiwa, Mbita visiwa vya Remba na Mfangano, zote zinazopatikana Homa Bay.

“Wavuvi wamegundua kuwa kuuza utumbo humpa mvuvi pesa nyingi mno na pia si ngumu kuusafirisha kama samaki wenyewe kwa sababu uzani wake ni mwepesi,” akasema Bw Onditi.

Serikali na pia vyombo vingine vya kudhibiti uvuvi Ziwa Victoria, navyo vimekuwa vikifuatilia jinsi ambavyo biashara hiyo inavyoendelea kunoga. Hii ni baada ya kubainika kuwa biashara hiyo huendeshwa kiharamu katika Kaunti ya Homa Bay.

Kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawana leseni ya kushiriki biashara hiyo, wengine wamekamatwa na kupigwa faini kubwa. Mmoja wao mwenye umri wa miaka 29 kutoka Remba alitozwa faini ya Sh100,000 kwa kuuza utumbo bila leseni.

Bi Alice Ojiambo naye alikamatwa mnamo Agosti 8 katika kisiwa cha Remba na kupelekwa kortini Mbiga kwenye Kisiwa cha Rusinga. Alikiri makosa yake na kutumikia kifungo cha wiki tatu kwenye gereza la Homa Bay baada ya kushindwa kulipa faini aliyotozwa.

  • Tags

You can share this post!

ODM yaambia Jalang’o, waasi wenzake wakanyage nje

Hofu vibiriti ngoma watachukua waume msimu huu wa nyumbu...

T L