• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
ODM yaambia Jalang’o, waasi wenzake wakanyage nje

ODM yaambia Jalang’o, waasi wenzake wakanyage nje

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE kiongozi wa ODM, Raila Odinga amewaangushia mjeledi wabunge saba na madiwani wanne waasi wa chama hicho kwa kuidhinisha kutimuliwa kwao.

Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la ODM chini ya uongozi kinara huyo wa upinzani jana liliamuru kuanzishwa kwa mchakato wa kufurushwa kwa wanne kati ya wabunge hao.

Wao ni Mbunge wa Gem, Elisha Ochieng’ Odhiambo, Caroli Omondi (Suba Kusini), Phelix Odiwuor maarufu kama Jalang’o, Gideon Ochanda (Bondo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

“Watano hawa wanachukuliwa kuwa wamejiuzulu kutoka kwa ODM kwa misingi ya kushirikiana na kuunga mkono sera za chama hasidi. Kwa kufanya hivyo, wamekiuka hitaji la kipengele cha 11 (1) (e) cha katiba ya chama chetu na sehemu ya 14 (a) ya sheria ya vyama vya kisiasa ya 2011,” ODM ikasema kwenye taarifa iliyosomwa na mwenyekiti wa kitaifa John Mbadi baada ya mkutano wa NEC katika makuu makuu ya ODM, Nairobi.

“Kwa hivyo, chama kinaagizwa kuanzisha mchakato wa kuondoa majina yao kutoka kwa sajili yake mara moja,” akaongeza Bw Mbadi ambaye ni Mbunge Maalum akiandamana na maafisa wengine wa ODM.

Aidha, chama hicho kilifutilia mbali uteuzi wa madiwani wake wanne maalum wanaohudumu katika Bunge la Kaunti ya Kisumu kwa “kukiuka misimamo na sera za ODM.”

Wao ni Bi Caroline Opar, Bw Kennedy Ojwang’, Bw Peter Obaso na Bi Regina Kizito. Hata hivyo, NEC ilitoa adhabu nyepesi kidogo kwa wabunge wengine waasi kama vile, Mbunge wa Uriri Mark Nyamita, Paul Abour (Rongo) na Mbunge Mwakilishi wa Nairobi Esther Passaris.

“Watatu hao walijieleza kwa njia ya kuridhisha mbele ya Kamati ya Nidhamu na hivyo NEC imeamua kwamba watozwe faini na kisha wawasilishe barua ya kuomba msamaha,” ODM ikasema.

Nyamita na Abour waliagizwa kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja ndani ya muda wa siku 60 huku wakitakiwa kuwasilisha barua ya msamaha ndani ya siku saba kuanzia jana.

Wawili hao sawa na wenzao watano waliadhibiwa kwa kumtembelea Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi mnamo Januari mwaka huu na kuahidi kuunga mkono sera za muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Kwa upande wake, Bi Passaris alitozwa faini ya Sh250,000 na awasilishe barua ya kuomba msamaha ndani ya siku saba kuanzia jana. Hii ni baada ya Mbunge huyo, anayehudumu muhula wa pili, kukaidi msimamo wa ODM na Azimio la Umoja-One Kenya, wakati wa upigaji kura bunge kuhusu Mswada wa Fedha, 2023, sasa Sheria.

Mnamo Juni 18, 2023 Bw Passaris alikuwa miongoni mwa wabunge 172, wengi wao wakiwa wale wa mrengo wa Kenya Kwanza waliopiga kura na kupitisha mswada huo ulipendekeza nyongeza ya ushuru kwa Wakenya na kuanzisha ushuru mpya wa nyumba.

“Ningependa kufafanua hapa kwamba ningali mwanachama wa ODM na mfuasi sugu wa Baba Raila. Lakini naunga mkono mswada huu kwa sababu ya pendekezo hili litakalowezesha maelfu ya watu wangu wa Nairobi kupata nyumba bora za gharama nafuu,” Bw Passaris akasema.

Hata hivyo, wabunge hao walioadhibiwa na ODM wanaweza kutaka rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Jopo la Kutatua Mizozo Ndani ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) au hata mahakamani.

  • Tags

You can share this post!

‘Mizimu’ ya Shakahola yaandama mochari na...

Biashara ya utumbo wa samaki aina ya Sangara yanoga Homa Bay

T L