• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Biashara zatarajiwa kunoga Iddi ikinukia

Biashara zatarajiwa kunoga Iddi ikinukia

Na WACHIRA MWANGI

WAFANYABIASHARA katika Kaunti ya Mombasa wameeleza imani yao kwamba watavuna pakubwa kifedha mwezi huu mtukufu wa Ramadhan unapokaribia kukamilika na kupisha sikukuu ya Iddi wiki ijayo.

Waislamu wanatarajiwa kusherehekea Iddi Alhamisi wiki kesho baada ya kumaliza kufunga mnamo Jumatano kulingana na mwandamo wa mwezi. Serikali inatarajiwa kutangaza siku hiyo kama sikukuu ya kitaifa.

Mjini Mombasa, sikuu ya Iddi husheheni sherehe na shughuli nyingi za kibiashara, wazazi wakiwanunulia watoto wao zawadi na kusherehekea kwa kuwaalika ndugu na jamaa.

Baada ya kuondolewa kwa marufuku ya usafiri katika kaunti tano za Machakos, Nakuru, Kiambu, Kajiado na Nairobi, wafanyabiashara eneo la Mombasa wanatarajia kwamba biashara zao zitanoga na wateja wataongezeka.

Maduka makubwa ya kijumla kama Nawal, Mombasa Mall mtaa wa Mwembe Tayari na soko kongwe la Marikiti yameanza kushuhudia shughuli nyingi huku Waislamu wakiwanunulia watoto wao vyakula, nguo na viatu kama maandalizi ya mapema ya Iddi.

Watu wanaendelea kumiminika katika barabara za Biashara na Kibokoni ili kununua bidhaa kwa maandalizi ya sikukuu hiyo.nBi Koki Musau ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Marikiti alisema kwamba tangu mwaka jana, ameona mabadiliko kibiashara na anatarajia mapato makubwa Ramadhan inapotamatika.

“Nimefurahi kuona angalau biashara zinaimarika baada ya athari hasi ya janga la corona. Wanunuzi wanaongezeka kwa hivyo natarajia faida tele. Mwaka 2020 tuliteseka kwa kuwa wakati kama huu nchi bado ilikuwa imefungwa,” akasema Bi Koki.

Naye Bi Saum Ali ambaye Alhamisi alinunua dera nne kwa Sh1,000 alishukuru Mwenyezi Mungu na kusema mazingira ya kufanya biashara mwaka huu wa 2021 ni salama kuliko mwaka 2020.

“Tunapokaribia mwisho wa Ramadhan, tunabahati kwamba mwaka huu tumeruhusiwa kutembea kutoka eneo moja hadi jingine. Naendelea kununulia familia na marafiki zawadi,” akasema.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara kutoka jamii ya Maasai mjini Mombasa Samuel Mole pia alikiri kwamba biashara ni nzuri ila changamoto ni mvua inayokunya sana eneo hilo.

“Tunapata faida ya kuridhisha na biashara zinaendelea vyema. Changamoto pekee ni mvua ambayo imefanya iwe vigumu kwa wateja kufika nyakati zote,” akasema Bw Mole.

“Wiki tatu zilizopita tumekuwa tukichuma vyema hasa jioni wakati kuna msongamano wa magari. Tunapokaribia mwisho wa Ramadhan, tunawaomba Wakenya wazidishe ibada ili janga hili la corona lituondokee. Tunahitaji kuimarisha uchumi wetu,” akasema mfanyabiashara Duncan Zuche ambaye amewaajiri vijana watatu kumsaidia katika duka lake la nguo.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa vyakula kwenye soko la Marikiti Mohammed Ali naye alifurahia idadi ya wateja wanaomiminika sokoni humo, akikiri kwamba wengi wanatoka Nairobi na kaunti nyingine nne zilizofungwa.

“Tuna imani kwamba idadi ya wanaotembelea maduka yetu wataongezeka siku chache hizi zilizosalia kabla ya Ramadhan kuisha. Ombi letu ni kwamba wanunuzi watazidi kuwa wengi na tutapata faida tele,” akasema Bw Ali.

Maduka, misikiti na vituo vingi vya kibiashara vimekuwa vikiweka taa zinazotoa mwangaza wa kupendeza ili kuwavutia wateja maandalizi ya Iddi yakishika kasi.

  • Tags

You can share this post!

Hofu safari zikikwama Mto Athi sababu ya mamba

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Hukumu ya Zakatul Fitr na namna ya...