• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Bidco yazidi kupanua biashara zake barani Afrika

Bidco yazidi kupanua biashara zake barani Afrika

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Bidco Africa Ltd imeonyesha uwezo wake wa kujiendeleza barani Afrika hasa uwekezaji na ustawishaji wa viwanda.

Waziri Msaidizi wa Biashara (CAS) Bw David Osiany, alizuru kampuni hiyo ya Bidco Africa Ltd inayotengeneza sharubati na maji mjini Ruiru, na kupongeza wasimamizi kwa juhudi wanazofanya.

Alieleza kuwa ameridhika na jinsi kiwanda hicho kinavyotengeneza bidhaa zake ikiwemo kufuata maagizo yote ya Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa (KEBS).

“Nimeridhika kuona jinsi kiwanda hiki kilivyojiimarisha kwa kutengeneza bidhaa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na KEBS,” alisema Bw Osiany.

Alitaja ushirikiano wa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hasa wa Kenya na nchi jirani ya Tanzania kama njia mojawapo ya “kuinua uchumi wetu na wa nchi jirani”.

Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa katika kiwanda hicho cha Ruiru ni maji ya matunda – sharubati – chapa Jooz, na mengine aina tofauti, pamoja na maji safi ya kunywa.

Aliyasema hayo Jumatatu alipozuru kiwanda hicho na maafisa kadha kutoka wizara yake pamoja na maafisa wa ukaguzi wa bidhaa bora zinazotengenezwa viwandani.

Alieleza kuwa serikali inashauri viwanda vinavyowekeza nchini vifanye kweli kwa kutengeneza bidhaa zilizo na ubora wa hali ya juu.

“Serikali inawaalika wawekezaji waje hapa nchini lakini nao wawe tayari kutengeneza bidhaa zilizo bora zaidi,” alifafanua Bw Osiany.

Mwenyekiti wa Bidco Africa Ltd, Bw Vimal Shah, aliwahimiza wafanyabiashara wote popote walipo waje pamoja ili kushirikiana katika malengo yao ya kukuza uchumi.

Alieleza kuwa wakati nchi ilikumbwa na homa ya Covid-19, kampuni ya Bidco Africa ilipitia changamoto tele lakini iliweza kukabiliana na mawimbi mazito yaliyoikabili.

“Licha ya mambo kuwa magumu bado tuliendelea kujizatiti na kufanya kazi bila kusimamisha shughuli zetu. Hata wafanyakazi wetu waliendelea na kazi bila kusimama,” alisema Bw Shah.

Meneja Mkurugenzi wa KEBS, anayekadiria ubora wa bidhaa nchini, Bw Benard Nguyo, alisema ameridhika na jinsi kampuni ya Bidco inatengeneza bidhaa bora na kufuata sheria zote zilizowekwa.

“Tumeridhika na hali ilivyo katika kiwanda hiki kwa sababu kila bidhaa inayotengenezwa imefuata utaratibu uliowekwa,” alieleza Bw Nguyo.

Alitoa changamoto kwa wawekezaji wengine kufuata mfano huo wa kutengeneza bidhaa bora zitakazonunuliwa na wateja bila malalamiko yoyote.

You can share this post!

Nasa sinaswi tena

Austria wapepeta North Macedonia na kuvuna ushindi wao wa...