• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Bidco yazindua kiwanda kipya mjini Ruiru

Bidco yazindua kiwanda kipya mjini Ruiru

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ina mipango ya kuendelea kufufua viwanda vingine hapa nchini ili kuongeza nafasi za ajira kwa vijana.

Rais Uhuru Kenyatta amesema hivi karibuni viwanda 40 vitafunguliwa kote nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kuangazia ajenda nne kuu za serikali.

“Nchi hii inastahili kujivunia bidhaa zake ambazo zinaundwa hapa. Umefika wakati wa sisi wenyewe kujivunia mali yetu hapa,” amesema Rais Kenyatta.

Ameyasema hayo Alhamisi wakati wa uzinduzi wa kiwanda kipya cha Bidco Industrial Park mjini Ruiru.

Rais Uhuru Kenyatta (kati) akiwa na Vimal Shah. Picha/ Lawrence Ongaro

Kiwanda hicho amesema kitaajiri takribani zaidi ya wafanyakazi 5,000 kwa siku za hivi karibuni.

Amesema atafanya jinsi awezavyo kuona ya kwamba ameangamiza umaskini ambao umekuwa ni tatizo kubwa nchini.

Aidha, amefafanua ushirikiano wake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ni jambo muhimu kwa nchi kwa sababu utulivu wa nchi umedhihirika huku biashara zikinawiri kote nchini.

“Mimi Rais wa nchi hii ya Kenya, ningetaka kuona taifa la Wakenya wote walio na mwelekeo mmoja,” amesema kiongozi wa nchi.

Amesema hivi karibuni Kenya itakuwa na maeneo mawili – Eldoret na Juja (JKUAT) – ya kutengeneza vipatakilishi na hiyo itamaanisha Kenya inapiga hatua kubwa kiuchumi.

Amewataka viongozi wazingatie maendeleo na waepukane kabisa na “siasa za pesa nane.”

Amesema hivi majuzi alifungua kiwanda cha kuunda magari cha KVM mjini Thika, na ni hatua kubwa ya kimaendeleo.

“Kwa hivyo, magari yote za serikali yataundiwa hapa kwetu badala ya kuagiza kutoka nchi za nje,” amesema Kenyatta.

Kuhusu siasa, Rais amesema ni muhimu viongozi kusubiri hadi wakati mwafaka.

“Wale wanaotafuta uongozi wangoje hadi mwaka wa 2022 na wajue ya kwamba Mungu ndiye anajua ni nani atakuwa kiongozi,” amesema Rais.

Kinara wa ODM Bw Raila Odinga amepongeza juhudi ya serikali kufufua viwanda hapa nchini.

Umeme

Ameiomba serikali ihakikishe ada ya kulipia umeme katika viwanda imeshuka.

“Iwapo serikali itaruhusu ada ya chini nazo viwanda vitaongeza mapato zao kwa kiwango cha juu.

Mwenyekiti wa kiwanda cha Bidco Bw Vimal Shah amesema kiwanda hicho kimepiga hatua kubwa na kuenea katika nchi kadha za Afrika.

Amesema kiwanda hicho kipya cha Bidco Industrial Park kinaendeshwa na mitambo ya kisasa huku kikiwa na ushirikiano wa karibu wa (BidCoro), na kampuni moja kutoka Denmark na ingine ya Ufaransa.

Amesema watazidi kushirikiana na serikali kwa lengo la kuafikia ajenda nne kuu zilizopangwa hapo awali.

Naibu Rais Dkt William Ruto, amesema serikali itaendelea kufanya maendeleo kulingana na jinsi walivyoahidi raia wa Kenya.

Amesema serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba uchukuzi unarahisishwa ili bidhaa ziweze kusafirishwa haraka na kwa usalama.

Hafla hiyo imehudhuriwa na washikadau tofauti kutoka sekta tofauti kote nchini.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yateremka kwenye uorodheshaji wa Fifa

Kangemi Ladies walenga juu zaidi

adminleo