• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Biden ampigia simu Ruto kumshukuru kwa kutuma polisi Haiti

Biden ampigia simu Ruto kumshukuru kwa kutuma polisi Haiti

NA KEVIN CHERUIYOT

RAIS wa Amerika, Joe Biden, Jumanne usiku alizungumza kwa simu na Rais William Ruto, ambapo alimshukuru Rais kwa hatua yake kukubali Kenya kuongoza kikosi cha usalama cha kimataifa kukabili magenge ya uhalifu nchini Haiti.

Mazungumzo baina ya viongozi hao wawili yalifanyika saa mbili usiku na yalidumu kwa nusu saa.

Kando na suala la Haiti, Rais Biden alimshukuru Rais Ruto kwa kuandaa Kongamano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, ambapo Afrika ilitoa msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.

Mapendekezo yaliyotolewa yatawasilishwa katika Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi litakalofanyika Dubai, Novemba.

Viongozi hao wawili walisifia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ambalo lilipiga kura kuunga mkono ombi la Kenya kuongoza kikosi hicho.

“Rais Joe Biden alizungumza na Rais William Ruto wa Kenya leo (Jumanne) kwa kukubali wito wa kuongoza Kikosi cha Usalama cha Kimataifa (MSS) nchini Haiti. Walisifia hatua ya UNSC kuagiza kupelekwa kwa kikosi hicho, ili kuwasaidia raia wa Haiti, ambao wametesekea sana mikononi mwa wahalifu wabaya,” ikaeleza taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House.

Awali, Rais Ruto alikuwa ameliahidi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kwamba, Kenya imejitayarisha kurejesha amani kwa watu wa Haiti, kutokana na madhila ambayo wamekuwa wakipitia mikononi mwa wahalifu.

Kando na masuala ya Haiti na kongamano kuhusu mabadiliko ya tabianchi, viongozi hao pia walijadili kuhusu nafasi zaidi za kuendeleza usalama wa kikanda kwa kubuni nafasi mpya za uwekezaji, ajira na ustawi endelevu.

Tayari, Amerika imeahidi kukisaidia kikosi hicho kifedha kwa kutuma Sh14.7 bilioni.

  • Tags

You can share this post!

Kuria sasa atania kaunti za Mlima Kenya akizitaka zipunguze...

Ugaidi: Familia yataka jamaa arudishwe nchini

T L