• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Ugaidi: Familia yataka jamaa arudishwe nchini

Ugaidi: Familia yataka jamaa arudishwe nchini

BRIAN OCHARO NA FARHIYA HUSSEIN

FAMILIA ya mwanamume Mkenya anayezuiliwa Somalia kwa madai ya kusafirishia kundi la kigaidi la al-Shabaab silaha, inataka serikali ya Kenya imrudishe nchini ili ashtakiwe huku.

Zakariya Kamal Sufi Abashiekh, 28, alikuwa amekamatwa nchini Aprili kwa madai ya kusaidia Al-Shabaab nchini Somalia kupata silaha kutoka China.

Wiki iliyopita, aligonga vichwa vya habari alipotoweka, familia yake ikidai alitekwa nyara na watu wasiojulikana katikati ya mji wa Mombasa. Baadaye, idara ya ujasusi Somalia ikatangaza alikamatwa katika nchi hiyo akitaka kutorokea maeneo ambayo yamo chini ya udhibiti wa magaidi.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, babake, Bw Kamal Sufi, aliisihi serikali ya Kenya imrudishe mwanawe nchini ili kama kuna kosa lolote alilofanya, ashtakiwe na kuhukumiwa humu.

Babake anaamini Abashiekh alikamatwa Mombasa akapelekwa hadi Somalia na watu wasiojulikana.

“Ninaomba serikali imrudishe humu nchini ili ashtakiwe. Sitaki ashtakiwe katika nchi ya kigeni ambapo anaweza kuumizwa. Ninataka ashtakiwe Kenya, ambapo mashtaka dhidi yake yanaweza kuthibitishwa na anaweza kufungwa jela au kuachiliwa huru kwa kuzingatia ushahidi utakaokuwepo. Nitakubali matokeo yoyote ya kesi,” akasema.

Bw Kamal alipuuzilia mbali madai kwamba mwanawe alikuwa na ushirikiano wowote na magaidi.

Kulingana naye, Abashiekh hajawahi kuenda Somalia kwa hivyo habari zilipoibuka kwamba alikamatwa katika nchi hiyo, familia yake ilishtuka.

“Nilichanganyikiwa. Ninamjua mwanangu. Huwa niko naye kila wakati, na ninaweza kukuhakikishia hajawahi kuenda Somalia,” akasema.

Hata hivyo, alithibitisha kwamba Abashiekh alikuwa na biashara ya kusafirishia watu mizigo kutoka China.

“Angemsaidia mtu yeyote ambaye angetaka kuagiza bidhaa kutoka China, kisha analipwa kwa kazi yake. Sanasana angefanyia kazi wateja ambao walitaka kusafirisha mizigo mingi kwa mauzo ya jumla,” akaeleza.

Katika mojawapo ya vikao vya mahakamani awali, mshukiwa huyo alikuwa ameambia mahakama ni kweli alikuwa na biashara aina hiyo.

Abashiekh anaaminika alianzisha biashara hiyo alipokuwa mwanafunzi wa Sayansi ya Masuala ya Kompyuta katika chuo kikuu kilicho China.

Hata hivyo, alikanusha mahakamani kwamba alikuwa na ushirikiano wowote na magaidi ambao anadaiwa aliwasafirishia zana za kivita.

Wiki iliyopita, familia yake ilidai kuna uwezekano alitumiwa vibaya na mabwanyenye ambao sasa wanataka atokomee.

Kulingana na babake, kabla Abashiekh akamatwe, alikuwa na duka la mapambo na bidhaa nyinginezo katika soko la Marikiti, katikati ya mji wa Mombasa.

Babake alisema yeye ndiye alimwanzishia biashara hiyo alipokamilisha masomo yake China.

Kijana huyo alisomea Shule ya Msingi ya Arya kabla kujiunga na Shule ya Upili ya Mvita mjini Mombasa, ambapo alipata alama ya C kwenye KCSE mnamo 2012.

  • Tags

You can share this post!

Biden ampigia simu Ruto kumshukuru kwa kutuma polisi Haiti

Baba azuiliwa kwa madai ya kupiga na kuua bintiye...

T L