• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Kuria sasa atania kaunti za Mlima Kenya akizitaka zipunguze mbio za kutimua magavana

Kuria sasa atania kaunti za Mlima Kenya akizitaka zipunguze mbio za kutimua magavana

NA LABAAN SHABAAN

WAZIRI wa Biashara Moses Kuria amesikitikia eneo la Mlima Kenya, akiwataka madiwani wapunguze mbio za kutimua magavana katika kaunti za eneo hilo.

Kauli yake ambayo alichapisha kwa mtandao wa X, inajiri huku madiwani wa Kaunti ya Meru wakiendelea kuongeza kuni kwenye tanuri la moto, kumbandua Gavana Kawira Mwangaza.

Akisema kanda hiyo imeingia katika historia kuwa na kaunti ya kwanza (Kiambu) kumfurusha gavana mamlakani kikamilifu, Bw Kuria alibainisha sasa ni wakati wa Mlima Kenya kuruhusu kaunti za maeneo mengine kuogelea kwa bahari hiyo chafu.

“Kwa moyo wa ujumuishaji na utangamano wa kitaifa, Mlima Kenya uachie nafasi kaunti nyingine kuwaondoa magavana wao,” waziri Kuria alionekana kutania, kauli yake ikionekana kumuunga mkono Gavana Mwangaza.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu aling’atuliwa uongozini na wawakilishi wadi, uamuzi uliopigwa muhuri na seneti Januari 2020.

Gavana huyu wa muhula wa kwanza aliondolewa kwa shutuma za ukiukaji wa katiba, jinai na utumizi mbaya wa mamlaka.

Akirejelea mzozo unaotokota kati ya wawakilishi wadi wa Meru na gavana Mwangaza, Bw Kuria anahofia wimbi la kuwatimua magavana eneo la Kati linaendelea.

“Katika muhula huu, Kaunti ya Meru inajizatiti kuwa kaunti ya kwanza kumuondoa gavana kikamilifu,” waziri Kuria aliendelea.

Hoja ya pili ya kujadili maadili ya Bi Kawira Mwangaza inatarajiwa kuwasilishwa katika bunge la kaunti ndani ya majuma mawili yajayo.

Ijapokuwa ilianguka hatimaye, hoja ya kwanza ya kumfurusha Gavana Mwangaza, ambaye haonani uso kwa macho na naibu wake Isaac Mutuma, ilisukumwa na diwani wa Abogeta Magharibi Denis Kiogora.

Kwa moto uo huo, wengi wa wawakilishi wadi wanampinga gavana kwa kuendeleza mpango wa Okolea Kaana ka Meru (Okoa mtoto wa Meru) ambao huwasambaza mashinani bidhaa kama vile magodoro, blanketi, mavazi, mifugo kama ng’ombe na kadhalika.

Magavana wengine waliotimuliwa na madiwani bila ufanisi ni Bi Anne Waiguru (Kirinyaga), Martin Wambora (Embu) na Paul Chepkwony (Kericho).

Mwaka 2021, Gavana wa Wajir Mohamed Abdi Mahmoud alikuwa gavana wa tatu kupoteza kiti chake mikononi mwa wajumbe wa kaunti baada ya Ferdinand Waititu na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko.

Hivi punde zaidi, Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo aliponea kubanduliwa alipolaumiwa na sehemu ya wawakilishi wadi kwa ufisadi na mapendeleo katika kutoa nafasi za ajira.

Madiwani 18 wa Nyamira walipiga kura kupinga hoja hiyo huku 16 wakiunga mkono.

Hoja ya kumfurusha Gavana Nyaribo ilihitaji madiwani 23 kuiunga kwa mujibu wa katiba ili ijadiliwe na Bunge la Seneti.

  • Tags

You can share this post!

Wito kwa walioambukizwa HIV wajitokeze waziwazi kuepusha...

Biden ampigia simu Ruto kumshukuru kwa kutuma polisi Haiti

T L