• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Bobi Wine anyakwa muda mfupi baada ya kurejea Uganda

Bobi Wine anyakwa muda mfupi baada ya kurejea Uganda

NA WANDERI KAMAU

CHAMA kikuu cha Upinzani nchini Uganda, Alhamisi, Oktoba 5, 2023 kilisema kuwa  kiongozi wake, Bobi Wine, alikamatwa na kuzuiliwa mara tu baada ya kuwasili nchini humo kutoka ziarani ng’ambo.

Hata hivyo, polisi baadaye walisema walimsindikiwa kiongozi huyo hadi katika makazi yake.

Bobi Wine (aliyekuwa mwanamuziki kabla ya kujitosa kwemye ulingo wa siasa), aliwasili katika Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Entebbe, Alhamisi asubuhi, baada ya kufanya ziara katika nchi kadhaa, ikiwemo Afrika Kusini.

“Kiongozi wetu [Bobi Wine] alichukuliwa na vikosi vya usalama mara tu baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege,” akasema David Lewis Rubongoya, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa chama cha National Unity Platform (NUP) kwenye mtandao wa ‘X’.

Ujumbe wake uliambatanishwa na picha  iliyoonyesha wanaume wawili wakimkamata.

Baadaye, polisi walitoa taarifa wakisema,  “Bobi Wine alisindikizwa na vikosi vyetu kutoka Entebbe hadi nyumbani kwake katika eneo la Magere. Alifika kwake mwendo wa saa tano asubuhi, ambapo kwa sasa yupo pamoja na familia yake na marafiki wake. Puuzeni vumi zinazoenezwa kwamba amekamatwa.”

Duru zilieleza kuwa wafuasi wa kiongozi huyo walikuwa wamepanga kumlaki kishujaa, na baadaye kuandamana naye hadi katika jiji kuu, Kampala.

Hata hivyo, polisi walitaja mikusanyiko ya umma kuwa marufuku.

Bobi Wine amekuwa akionekana kuwa mwiba sugu kisiasa kwa serikali ya Rais Yoweri Museveni.

Mnamo 2021, aliwania urais kumkabili Museveni, anayehudumu kwa muhula wa sita kama Rais, japo akaibuka wa pili.

Licha ya umri wake mkubwa, Museveni amesema atawania urais tena 2026.

  • Tags

You can share this post!

Kombe la Afrika: Janet Okello awasili kutoka Japan kupiga...

Makanisa ya kiasili yalia kutelekezwa na wanasiasa baada ya...

T L