• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Makanisa ya kiasili yalia kutelekezwa na wanasiasa baada ya uchaguzi

Makanisa ya kiasili yalia kutelekezwa na wanasiasa baada ya uchaguzi

NA TITUS OMINDE

Makanisa ya kiasili ambayo yalichangia pakubwa juhudi za Rais William Ruto za kuingia Ikulu mwaka 2022 kwa kukumbatia simulizi yake ya ‘Bottom Up’ sasa yanamshutumu Rais na kikosi chake cha Kenya Kwanza kwa kuwatelekeza na kupendelea makanisa yanayopata ufadhili kutoka ng’ambo.

Viongozi wa makanisa hayo sasa wanadai kuwa hawaoni wanasiasa kutoka Kenya Kwanza wakiungana nao katika ibada zao kwani ilikuwa ni kawaida wakati wa msimu wa kampeni kuona wanasiasa hao kanisani mwao.

“Wakati wa kampeni za 2022 wanasiasa wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Rais Ruto walijigeuza kama waumini wa makanisa yetu kwa kuhudhuria ibada zetu na baada ya kupanda Ikulu wametutelekeza,” alisema Askofu Mkuu John Chabuga wa kanisa la African Devine Church (ADC).

Wakati wa ziara za nchi nzima, akiwa na washirika wake wa karibu, walisafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine, kanisa moja hadi lingine na kiasi kikubwa cha michango kila Jumapili.

Akizungumza na Taifa Leo Askofu Chabuga alisema ni bahati mbaya kwamba wanasiasa na viongozi wengine walithamini makanisa yao tu wakati wa kampeni lakini kwa sasa wamehamia katika makanisa makubwa ya kifahari.

“Tunatoa wito kwa wanasiasa ambao walikuwa wakitembelea makanisa yetu wakati wa kampeni kuendelea kuja makanisani kwetu na kuunga mkono mipango yetu ya maendeleo. Ni vibaya kuthamini makanisa tu wakati wa kampeni,” alisema Askofu Chabuga.

Askofu Chabuga alimsihi Rais Ruto na wanasiasa wote kutoka Kenya Kwanza kuja kwa ajili ya maombi katika makanisa yao na kuchangia miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, aliwataka wafuasi wake kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya serikali ya Kenya Kwanza bila ya ubaguzi.

Kwa upande wake Askofu John Pesa wa Kanisa la Holy Ghost Coptic, alisema katika kipindi cha kampeni makanisa yao yalidhaminiwa sana na hata kupokea mialiko ya kutembelea nyumbani kwa Rais Ruto eneo la Sugoi lakini kwa sasa wamesahaulika.

“Wanasiasa ni watu wa kubembeleza sana wanapotaka kura zetu watapiga magoti hata kwenye sakafu zetu zenye vumbi lakini baada ya kupata wanachotaka, hutawaona kamwe,” alisema Askofu Pesa.

Askofu Pesa alisema siku hizi hapokei simu kutoka kwa wanasiasa wanaotaka kuhudhuria ibada kanisani mwake kama ilivyokuwa wakati wa kampeni.

Askofu Pesa ambaye hisia zake zilisambaa mnamo Oktoba 14, 2020 baada ya kulalamikia ada ya ‘udhamini mdogo’ kutoka kwa Rais Ruto alipokuwa Naibu Rais alionya Wakenya dhidi ya kuamini wanasiasa.

Akizungumza baada ya kumtembelea Ruto nyumbani kwake Sugoi mwaka wa 2020, Askofu Pesa alidai kuwa alilipwa pesa duni, na waandalizi wa hafla husika huku baadhi ya wenzake wakilipwa vizuri.

Alibainisha kuwa alipokea Sh 10,000 tu ambayo ilikuwa chini ya matarajio yake kwa kuzingatia gharama aliyotumia kusafiri kutoka Kisumu hadi Sugoi.

Katika kipindi cha kampeni, Rais Ruto alikuwa amejitolea sana kanisani kwani aliahidi kulinda taasisi za kidini iwapo atachaguliwa kuwa Rais Agosti 9.

Akitafuta kura wakati wa kampeni aliwahakikishia viongozi wa makanisa kuhusu kujitolea kwake kulinda uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba.

  • Tags

You can share this post!

Bobi Wine anyakwa muda mfupi baada ya kurejea Uganda

Aaron Cheruiyot ataka maafisa waliozembea kuzima mapigano...

T L