• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Bunge kuandaa kikao cha pamoja kwa mdahalo kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Bunge kuandaa kikao cha pamoja kwa mdahalo kuhusu mabadiliko ya tabianchi

NA CHARLES WASONGA

BUNGE Jumatano, Septemba 6, 2023, litaandaa Mdahalo wa Wabunge kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi Afrika katika Majengo ya Bunge jijini Nairobi.

Kikao hicho cha pamoja cha maseneta na wabunge, na kisicho rasmi, kitaongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Spika wa Seneti Amason Kingi.

Wabunge na maseneta wako likizoni na hivyo vikao vya kawaida vimesitishwa isipokuwa vile vya kamati za mabunge hayo mawili.

Kwenye taarifa Jumanne, Bw Wetang’ula na Bw Kingi walisema wabunge na maseneta kutoka Kenya na nchi za kigeni, wanaohudhuria Kongamano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, wamealikwa kushiriki mdahalo huo.

Maspika hao walisema mabunge ni nguzo katika kusukuma maafikiano kuhusu mbinu za kutumia uwezo na rasilimali za Afrika katika kukabili athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mabunge yana uwezo wa kuzindua nchi za Afrika na dunia kwa ujumla kutumia nafasi zilizopo kupunguza uchafuzi wa hewa na mazingira pamoja na kuhimiza matumizi ya kawi safi na endelevu,” taarifa ya Mbw Wetang’ula na Kingi ikasema.

“Hii ndio maana kama asasi za kutunga sheria pia tuko mtari wa mbele kusukuma serikali zitenge pesa za kutosha kwa mipango ya kupunguza makali ya tabianchi. Hii ndio maana mdahalo wa Jumatano ni muhimu zaidi,” taarifa ikaeleza.

Kongamano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (ACS23) linafanyika kwa mara ya kwanza Afrika huku Kenya ikiwa mwenyeji.

Kongamano hilo chini ya kauli mbiu; “Kuendeleza Matumizi ya Nishati Safi na Ufadhili wa Mikakati ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Afrika na Ulimwengu” linakamilika Jumatano, Septemba 6, 2023 katika jumba la KICC, Nairobi.

Rais William Ruto ndiye mwenyeji wa kongamano hilo chini ya wadhifa wake kama Mshirikishi wa Marais wote wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi katika Umoja wa Afrika (AU).

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika kongamano hilo ni jinsi ya kuzuia utoaji wa hewa mbaya angani, uwekezaji katika viumbe asili, suluhu kwa mabadiliko ya tabianchi na ufadhili wa mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi Mlima Kenya waendeleza uhasama dhidi ya wanahabari

Nimeganda kwa mume wa mtu, nitajitoaje?

T L