• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Viongozi Mlima Kenya waendeleza uhasama dhidi ya wanahabari

Viongozi Mlima Kenya waendeleza uhasama dhidi ya wanahabari

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua tangu atoe matamshi ya kuwakaripia wanahabari, ameigwa na wenzake katika siasa na maafisa wa polisi katika eneo la Mlima Kenya, haswa Kaunti ya Murang’a.

Bw Gachagua amenukuliwa mara si moja akiwarejelea wanahabari kuwa baadhi yao wamekosa dira.

Alienda hatua zaidi kudai kwamba  waliunga kinara wa upinzani Bw Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Sasa wenzake wamekuwa katika mbio za kumuiga.

Akiwa katika kaunti ndogo ya Gatanga mnamo Februari 23, 2023, Bw Gachagua alisema kwamba “hawa waandishi wa habari wamefadhiliwa na wakora wa sekta ya maziwa na pia wao ni wa Azimio”.

Baadaye akiwa katika mahojiano na vituo kadhaa vya runinga katika makao rasmi ya Karen, Bw Gachagua alisema kwamba “hao waandishi huwa wanaingia kazini wakiwa walevi na wakiwa na nia ya kushambulia viongozi katika mikutano”.

Hata hivyo, hakutoa ushahidi kwamba aliowarejelea kama walevi kweli wanalewa.

Waziri wa Biashara na Viwanda naye akachafua hewa kwa kuwarejelea wanahabari kuwa hawana maadili.

“Hawa nitamenyana nao vile walivyo… Nitawashikia kwa pembe nanyi mshike mateke,” akasema mnamo Julai 24, 2023.

Nao wasaidizi wa mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua mnamo Agosti 19, 2023, katika uwanja wa Kimorori, walimvamia mwandishi wa habari Bi Muthoni Gitau na kumpiga.

Hawakujali kwamba Bi Gitau hufanya kazi katika kituo cha utangazaji cha serikali cha KBC ambapo huwajibikia kituo cha Coro FM kinachotangaza kwa lugha ya Gikuyu.

“Waliniambia kwamba sikufaa kuhudhuria mkutano uliokuwa umepangwa na mbunge huyo kwa kuwa huwa simuungi mkono. Niliwauliza kama wako na uhakika wako na mamlaka ya kuamua ni mwandishi gani atahudhuria hafla za umma na ndipo wanaume wawili walinishambulia,” akasema Bi Gitau.

Mnamo Septemba 1, 2023, maafisa wa polisi waliokuwa katika doria mjini Kenol katika kaunti ndogo ya Murang’a Kusini, walimshambulia kwa rungu Bw Joseph Wachira ambaye hufanyia kazi kampuni ya Royal Media Services (RMS).

“Nilikuwa nimepigiwa simu na wakazi katika eneo moja la mji huo ambapo tetesi zilikuwa kwamba maafisa hao walikuwa wakipiga watu kiholela na kuwapora. Kufika hapo nilipata ni ukweli na katika hali ya kuhoji baadhi ya waathiriwa, nilishtukia nimepigwa rungu kwa mkono wangu wa kulia,” akasema.

Bw Wachira alikimbizwa hospitalini ambapo mkono wake uligunduliwa kupasuka mishipa kadha.

Mkuu wa polisi wa Murang’a Kusini Bi Jane Nyakeruma alikataa kuongea na Taifa Leo kuhusu kisa hicho.

Katika kisa cha  Septemba 1, 2023, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti hiyo Bi Betty Maina alitumia maneno yanayosawiriwa kama lugha chafu dhidi ya mwanahabari wa kampuni ya Standard Bw Boniface Gikandi.

Bi Maina bila kutoa ushahidi wowote, alienda hatua moja zaidi kwa kudai kwamba Bw Gikandi huwa anamchumbia kimahaba na akikataliwa, humdai Sh100,000 kama kitulizo.

Ghadhabu ya Bi Maina ilitokana na stori ambayo Bw Gikandi alikuwa ameandika katika gazeti la siku hiyo ikisema kwamba kuna wasiwasi kwamba pesa za maendeleo za eneobunge la Mathira zinatumika katika Kaunti ya Murang’a.

Bi Maina ni mke wa mbunge wa Mathira Bw Eric wa Mumbi.

Bi Maina alizidisha mashambulio yake kwa kudai kwamba “tulimchangia kumwokoa alipokuwa anaugua lakini haandiki mema kutuhusu”.

Wengi wa waandishi hao sasa wameingiwa na hofu kwamba kuna mpango ulio wazi wa kuwalenga kupitia siasa za uongo, propaganda na pia kupitia ufadhili wa magenge ya kuwashambulia pamoja na maafisa wa polisi.

“Ingawa ni vigumu waandishi wa habari wanaojielewa waingize baridi kutokana na njama hizo za kipuzi, ni vyema ieleweke kwamba tabia hizo za wanasiasa na maafisa wa polisi haziambatani kamwe na katiba ambayo ndiyo imetoa nafasi ya taaluma ya uanahabari kuchukua nafasi yake katika jamii pasipo mwingilio wa kutoka kwa yeyote,” akasema Bw Wachira.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto amuomboleza Muthoni wa Kirima kama shujaa...

Bunge kuandaa kikao cha pamoja kwa mdahalo kuhusu...

T L