• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
CBC: Sossion awasilisha malalamiko ya wazazi bungeni

CBC: Sossion awasilisha malalamiko ya wazazi bungeni

Na FAITH NYAMAI

BAADHI ya wazazi wamewasilisha ombi katika Bunge la Kitaifa wakitaka kusitishwa kwa utekelezaji wa Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) nchini ili wanafunzi warejelee mfumo wa elimu wa 8-4-4.

Ombi hilo lililowasilishwa na Mbunge Maalum Wilson Sossion ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Nchini (Knut), linadai utekelezaji wa CBC unakiuka sheria.

Wazazi hao wanapendekeza kushtakiwa kwa maafisa wa serikali ambao wamekuwa wakiendeleza utekelezaji wa mtaala huo mpya, wakidai wanavuruga ubora wa elimu nchini.

Akisoma ombi hilo bungeni Alhamisi, Bw Sossion alisema CBC iliyozinduliwa mnamo 2017 inawahitaji walimu kuandaa mwongozo wa masomo na kuwatathmini wanafunzi.

“Walimu pia wanahitaji kubadili mifumo mingine ya ufunzaji kutoka ule wa kawaida hadi ule unaohusu utendaji katika masomo,” akaeleza.

Pia ombi hilo linasema kuwa CBC inahitaji walimu kubadili kutoka wajibu wao wa kuwa wataalamu hadi watu wa kutoa mwongozo kuhusu utaratibu wa masomo.

Kulingana na wazazi hao, sehemu ya 41 ya Sheria ya Elimu ya Msingi nambari 4 ya 2013, inatambua mfumo wa 8-4-4 ndio unapaswa kufunzwa katika shule za Kenya na kwamba sheria hiyo haijadilishwa.

“Ni kwa sababu hiyo ambapo tunasema utekelezaji wa CBC unakiuka Katiba,” wanasisitiza.

Walalamishi hao wanasema kuwa mtaala huo haukupangwa vizuri na ulianzishwa haraka katika shule za humu nchini pasina na kuzingatia uwepo wa changamoto ya ukosefu wa rasilimali za kufanikisha utekelezaji wake.

“Kutokana na hilo, wajibu wa walimu katika utayarishaji wa mipango ya mitaala umekuwa finyu. Vile vile, kuna vipengele vingi vyenye utata ambavyo vimegeuza CBC kuonekana kama mtaala wa matajiri,” Bw Sossion akasema katika maelezo yake, alipowasilisha ombi hilo.

Alisema uchunguzi uliofanywa hivi punde ulionyesha kuwa shule nchini hazijajiandaa ipasavyo kwa utekelezaji wa mtaala wa CBC ambao unachukua nafasi ya mfumo wa 8-4-4.

Bw Sossion pia anasema kuwa utekelezaji wa CBC ulianzishwa kabla ya walimu wengi kupewa mafunzo tosha kuhusu vipengele vyake na mbinu za kufunza katika mfumo huo.

You can share this post!

BERLIN MARATHON: Waethiopia wang’ara

DINI: Unahitaji hekima kucheza karata zako vyema maishani...