• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Chama chakana Wajackoyah ataburudisha Nyeri

Chama chakana Wajackoyah ataburudisha Nyeri

NA MERCY MWENDE

CHAMA cha Roots kimepuuzilia mbali ripoti kwamba mgombea wake wa urais George Wajackoyah anatarajiwa kuzuru mji wa Nyeri wikendi hii kwa shoo ya ‘reggae night’ katika kilabu kimoja cha burudani.

Akiongea na Taifa Leo, msemaji wa chama hicho Wilson Muirani, maarufu kama Jaymo Ule Msee, alikana madai ya kiongozi wa chama hicho ameratibiwa kukutana na wafuasi wake leo Jumamosi.

Kulingana na bango linalozungushwa katika mitandao ya kijamii, Prof Wajackoyah alikuwa amepangiwa kuhudhuria tamasha la ‘reggae night’ katika Joy Green Resort, viungani mwa mji wa Nyeri.

Ripoti kuhusu tamasha hilo ilizuzua mashabiki wengi wa burudani katika mitandao ya kijamii kwa muda wa wiki moja sasa.

Kulingana na tangazo katika mabango hayo ni watu wenye umri wa miaka 21 kwenda juu pekee ndio walihitajika kuhudhuria tamasha hilo kwa ada ya kiilingilio ya Sh300, kila mmoja.

Lakini kulingana na Bw Muirani, shughuli hiyo iliyovumishwa zaidi mitandaoni ni feki, na wanachama wa chama cha Roots hawana habari kuihusu.

“Ama kwa kweli, tumeona tangazo hilo katika mitandao ya kijamii sawa na watu wengine na tukashangaa. Tujuavyo ni kwamba mgombea urais kwa tiketi ya chama chetu hana mipango ya kuzuru eneo la Kati mwa Kenya wikendi hii,” akasema.

Bw Muirani alisema tamasha hilo liliandaliwa na walaghai ambao nia yao ilikuwa kuchuma pesa kutoka kwa wananchi kwa njia haramu.

  • Tags

You can share this post!

Matajiri Mlimani wakariri imani yao kwa Raila

TAHARIRI: Mtindo wa serikali kuchelea kufadhili timu za...

T L