• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Chiloba mtetezi wa ‘LGBTQ’ alikuwa Mkristo thabiti – Familia

Chiloba mtetezi wa ‘LGBTQ’ alikuwa Mkristo thabiti – Familia

FRED KIBOR Na BARNABAS BII

HUKU polisi wakiwakamata washukiwa wengine wanne kuhusiana na mauaji ya mwanaharakati wa ushoga Edwin Kiptoo Chiloba, familia yake sasa inasema alikuwa Mkristo thabiti.

Kwa mujibu wa binamu yake, Caustencia Tanui, wameshangazwa na mauaji yake na ufichuzi kuwa alikuwa shoga ilhali walimjua kama mtu mcha Mungu.

“Kulingana na sisi, alikuwa Mkristo na hata akiwa mwanafunzi katika Shule ya Upili ya St Francis, Kimuron, alikuwa mwanachama wa muungano wa Wanafunzi Wakristo. Alikuwa mwanafunzi aliyependa kuomba kila mara. Mauaji yake yametushtua. Hata kama alikuwa shoga alifaa kuendelea kuishi. Hatutapumzika hadi haki itakapopatikana,” akaambia Taifa Leo.

Bi Tanui alifichua kuwa binamu yake alijulikana kama mtu mwadilifu tangu utotoni mwake na alipashwa tohara kulingana na tamaduni za jamii ya Wakalenjin.

Alisema baadhi ya watu wa rika lake bado hawajaamini ufichifuzi kuwa alikuwa shoga.

Hata hivyo, Bi Tanui alishuku huenda mienendo ya Chiloba ilibadilika alipojiunga na Chuo Kikuu cha Eldoret.

“Awali, alikuwa akisoma kozi ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Eldoret lakini akabadili kozi hiyo na kuamua kusomea taalamu ya Mitindo ya Mavazi. Dada zake walikuwa wakimlipia karo walipinga vikali uamuzi huo,” akasema.

Wakati fulani Chiloba alikatiza masomo kutokana na uhaba wa karo.

“Lakini baada ya muda tuligundua kuwa alipata mfadhili na kurejelea masomo,” Bi Tanui akaeleza.

Bi Tanui aliongeza kuwa mwendazake alionekana nyumbani kwao, Sergoit, Elgeyo Marakwet, mara ya mwisho miaka miwili iliyopita.

“Na tulipomuuliza kwa nini hakutembea nyumbani kwa muda mrefu, alidai kuwa alibanwa na shughuli za shoo yake ya mitindo ya mavazi, ikiwemo hafla ya Kitenge Fest iliyokamilika juzi. Tulimpenda kwa sababu alituonyesha picha nyingi za hafla hiyo,” akasema.

Bi Tanui alidai kuwa Chiloba aliuawa kwa sababu ya pesa kwani mfadhili wake kutoka ng’ambo alikuwa amemtumia Sh125,000 kulipia karo.

Zaidi ya hayo, alisema marehemu alikuwa amepata mkataba wa thamani ya pesa nyingi wa kusanifu mavazi aina ya vitenge.

“Maiti yake itafanyiwa upasuaji Jumatatu (leo) na tunapanga kumzika katika shamba la babake eneo la Sergoit, Elgeyo Marakwet Jumamosi,” Bi Tanui akafichua.

Mkuu wa kitengo cha ujasusi kaunti ya Uasin Gishu Peter Kimulwa alisema kwamba washukiwa wawili zaidi walikamatwa Jumamosi jioni.

“Washukiwa, Ramsey Chepwao, 17, Jaen Ochieng, 19, binamu ya mshukiwa mkuu Emmanuel Omondi sasa wanazuiliwa katika korokoro ya polisi kuhusiana na mauaji ya Chiloba,” akasema Bw Kimulwa.

  • Tags

You can share this post!

Ni mambo mapya Ikulu enzi ya Ruto

Raila ataka Ruto amtafute ikiwa anataka kubadili Katiba

T L