• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Raila ataka Ruto amtafute ikiwa anataka kubadili Katiba

Raila ataka Ruto amtafute ikiwa anataka kubadili Katiba

NA WINNIE ATIENO

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga amemtaka Rais William Ruto kushauriana na Wakenya na viongozi wa upinzani kuhusu mipango yoyote ya mageuzi ya katiba anayopanga kuanzisha.

Bw Odinga alisema Rais haweze kuwapeleka mawaziri bungeni kwa kubadilisha sheria za bunge, akisema hatua hiyo ni sawa na kubadilisha mfumo wa uongozi “tulio nao wakati huu”.

“Suala hilo sharti lijadiliwe kwa kina na watu wa Kenya. Akitaka kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu, pendekezo hilo liko katika mswada wa mpango maridhiano (BBI). Mbona unamwita Mkuu wa Mawaziri? Mwite Waziri Mkuu na mpe wizara atakayosimamia. Ninamhurumia Bw Musalia Mudavadi kwa kuwa mtu wa hadhi yake amekosa wizara, ni jina tu. Hii ni aibu kubwa,” akasema.

Aidha, Bw Odinga amemtaka Rais Ruto kushauriana na viongozi wa upinzani na Wakenya kuhusu matukio yaliyojiri katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi wakati wa kujumuishwa kwa kura za urais baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Akiongea Jumapili wakati wa ibada katika Kanisa la Anglikana (ACK) jijini Mombasa, Bw Odinga alisema Wakenya wanataka kujua ukweli.

“Sitaki kushiriki malumbano yoyote na Bw Ruto kwani anajua fika kwamba yote anayopendekeza yako katika mswada wa BBI. Akitaka tuongee, tuanzie hapo. Sharti ashauriane na Wakenya kuhusiana na mabadiliko yoyote ya Katiba ambayo anataka kuleta,” akasema.

Kiongozi huyo wa Azimio la Umoja-One Kenya alipendekeza kuwa ukaguzi wa matukio hayo ya ujumuishaji wa kura sharti uanze kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati.

Kwa mara nyingine, Bw Odinga alisisitiza kuwa sharti Bw Chebukati ashtakiwe kwa makosa ya uhalifu wa kibinadamu katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), jijini The Hague, Uholanzi.

“Alitoweka kwa muda katika ukumbi wa Bomas of Kenya. Kisha akatokea na kutangaza matokeo. Alipata wapi matokeo hayo?” akauliza huku akiongeza kuwa hivi karibuni atafichua yaliyotokea katika ukumbi wa Bomas.

Bw Odinga alisema kubainika kwa ukweli kuhusu uchaguzi wa urais wa 2022 kutasuluhisha shida inayokumba Kenya “kwa sababu Wakenya watajua aliyeshinda na aliyepoteza katika uchaguzi huo.”

Pia alikana ufichuzi wa Rais Ruto kwamba kulikuwa na jaribio la mapinduzi ya serikali wakati wa uchaguzi huo wa urais.

Bw Odinga alisema mapinduzi hufanywa dhidi ya serikali iliyoko mamlakani, akiongeza kuwa jeshi halingefanya mapinduzi dhidi yake mwenyewe.

“Huo ni uwongo. Serikali ingefanyaje mapinduzi dhidi yake? Wangetaka kufanya mapinduzi, nani angewazuia? Rais Kenyatta alisema alitaka uchaguzi huru na haki na kuwa serikali haingeingilia shughuli hiyo kwa njia yoyote ile. Kilichotokea ndicho Wakenya wanataka kujua. Ni mwenyekiti wa IEBC aliyefanya mapinduzi ya kiraia, nne dhidi ya tatu,” akaongeza.

Bw Odinga akaendelea; “Makamishna wanne walisema hawakukubaliana na Bw Chebukati, ilhali alisisitiza kuwa alikuwa na matokeo halali. Jiulize nani anasema ukweli. Suala hilo ndilo nitazungumzia. Kile Wakenya sharti wajue ni kwamba hakuna haja ya wao kushiriki uchaguzi wa 2027 utakaoendeshwa kwa njia tulioshuhudia katika Bomas of Kenya.”

Alisema aliungana na waumini wa Kikristo jijini Mombasa katika ibada ya Jumapili ya kwanza ya mwaka huu mpya kuabudu nao na kuwahimiza vijana kuendelea kutenda mema katika jamii.

  • Tags

You can share this post!

Chiloba mtetezi wa ‘LGBTQ’ alikuwa Mkristo thabiti –...

Ruto kuzuru tena ngome ya Raila kwa hafla ya Owalo...

T L