• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
‘Corona’ ya punda yalipuka na kuzua hofu kubwa Lamu

‘Corona’ ya punda yalipuka na kuzua hofu kubwa Lamu

Na KALUME KAZUNGU

IDARA ya mifugo katika Kaunti ya Lamu imetoa tahadhari kwa umma kufuatia mkurupuko wa homa ya punda ambayo imeibua hofu miongoni mwa wakazi kisiwani.

Haijajulikana kama punda wanaweza kuambukiza binadamu ugonjwa huo ambao chanzo chake hakijabainika.

Dalili zinazoonekana ni kama vile matatizo ya kupumua, punda kutoa kamasi tele, na kuambukizana kwa kasi.

Kufikia Jumanne, zaidi ya punda 60 walikuwa tayari wameonyesha dalili za kuugua maradhi hayo.

Akithibitisha mkurupuko huo, Afisa Mkuu wa Idara ya Mifugo na Matibabu katika kaunti, Bw Gichohi Mathenge, alisema tayari wametoa sampuli ya damu na kamasi kutoka kwa baadhi ya punda wanaougua maradhi hayo na kuisafirisha jijini Nairobi kwa uchunguzi zaidi ili kubaini ni ugonjwa gani hasa.

Kwa sasa, aliwataka wenye punda kuwafikisha wanyama wao katika kituo cha matibabu ya punda mjini Lamu kwa uangalizi zaidi endapo watashuhudia wakipumua kwa shida.

“Kufikia sasa hakuna punda aliyefariki kutokana na maradhi hayo,” akasema Bw Mathenge.

Bw Abdallah Awadh ambaye humiliki punda na ni mshauri wa kituo cha matibabu ya punda katika kisiwa cha Lamu alieleza hofu yake kuhusiana na maradhi hayo.

Bw Awadh alisema wako tayari kushirikiana na matabibu wa mifugo ili kuona kwamba wanapata usaidizi wa kimatibabu kwa punda wao ili wasiangamie.

‘Mimi niko na zaidi ya punda 10 katika boma langu. Nimeshuhudia karibu punda watatu wangu wakiwa na shida ya kupumua juma hili. Wengine wamekuwa wakitoa makamasi mengi. Nilidhani ni homa tu ya kawaida lakini nashukuru kwamba idara ya mifugo iko mbioni kutambua aina hii ya ugonjwa kwa punda wetu,’ akasema Bw Awadh.

Mmiliki mwingine wa punda, Bw Salim Dere ambaye ni mmiliki wa punda kisiwani Lamu aliomba zoezi lililopangwa la kuwachanja punda wao kuharakishwa ili kuwakinga dhidi ya maradhi, ikiwemo yale yanayoibuka.

“Ombi langu ni kwamba maradhi haya yakabiliwe na kudhibitiwa haraka kabla hatujashuhudia punda wetu wakifariki. Bado hatujasahau hasara tuliyomadiria wakati punda wetu walipofariki katika hali tatanishi mwaka 2013,” akasema Bw Dere.

Haya yanajiri wakati ambapo idara ya mifugo imetangaza mpango wa kuwachanja karibu punda 4,000 Lamu dhidi ya kichaa na maradhi mengine. Shughuli hiyo imepangwa kutekelezwa juma lijalo.

  • Tags

You can share this post!

WASONGA: Vijana wahimizwe kujisajili kwa miradi ya...

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya...