• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Dkt Patrick Amoth Mkenya wa kwanza kupata chanjo ya corona

Dkt Patrick Amoth Mkenya wa kwanza kupata chanjo ya corona

Na SAMMY WAWERU

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini, Dkt Patrick Amoth amekuwa Mkenya wa kwanza kupata chanjo dhidi  ya virusi vya corona (Covid-19).

Dkt Amoth alipokea chanjo hiyo Ijumaa, kwa njia ya kudungwa sindano, katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), jijini Nairobi ambapo idara ya afya ilizindua rasmi waliolengwa kuanza kupokea.

Wahudumu wa afya, maafisa wa usalama, walimu ni kati ya watakaopewa kipau mbele kuchanjwa.

Akionekana mwingi wa uchangamfu, afisa huyo mkuu aliambia wanahabari kwamba alihisi uchungu kidogo tu wakati akidungwa.

“Haina uchungu. Nilihisi uchungu kiasi tu na ndio maana nimeweza kusimama mbele yenu kuwazungumzia,” Dkt Amoth akaelezea wanahabari, dakika chache kabla ya saa saba mchana baada ya kupata chanjo.

Alisema kabla ya kuchanjwa, alikuwa amearifiwa athari zinazoweza kutokana na chanjo hiyo.

“Nilikuwa nimeelezwa kuhusu athari zake kama vile kuumwa na kichwa…Ila si wote watakaozishuhudia. Athari ni tofauti, kulingana na maumbile ya mtu,” Dkt Amoth akasema.

Katibu katika Wizara ya Afya, Bi Susan Mochache ndiye alizindua rasmi waliolengwa kuanza kupata chanjo hiyo aina ya AstraZeneca na iliyotengenezwa katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.

Aidha, chanjo hiyo iliwasili nchini Kenya Jumanne usiku, na kupokewa na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta alizindua rasmi Alhamisi chanjo hiyo kuanza kusambazwa katika kaunti zote 47 nchini.

You can share this post!

Mwandishi wa NMG, Pauline Ongaji atuzwa

Wakenya washangaa mbona Uhuru, Ruto na Raila hawajapokea...