• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
EACC yaahidi kuchuja vikali wawaniaji 2022

EACC yaahidi kuchuja vikali wawaniaji 2022

Na ANTHONY KITIMO

WANASIASA wanaolenga viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao lazima watapitia ukaguzi wa kina kulingana na hitaji la katiba kabla ya kuidhinishwa kuwania nyadhifa hizo.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilisema Alhamisi kuwa hakuna mwanasiasa ambaye atasazwa katika ukaguzi huo ambao utalenga kuhakikisha kuwa wana maadili na wametimiza vigezo kuwania vyeo hivyo.

Mkurugenzi wa Huduma ya Kisheria David Ruto alisema mbali na kujaza fomu, tume hiyo itakuwa ikifanya uchunguzi wake kibinafsi kwa wawaniaji kutoka vyama mbalimbali.

“Wale ambao wanalenga uongozi wanafaa wafahamu kuwa mara hii hatutalegeza kamba kuhakikisha katiba inafuatwa. Kama EACC, tutafanya kazi pamoja na taasisi nyingine ili tupate viongozi bora,” akasema Bw Ruto.

“Tutahakikisha kuwa tumekabidhi IEBC ripoti na maelezo kuhusu wawaniaji wote kabla hawajaidhinishwa kuwania vyeo mbalimbali,” akasema Bw Ruto.

Alikuwa akizungumza jijini Mombasa alipozindua warsha ya wiki moja kuhamasisha umma kabla ya Disemba 9 ambayo ni Siku ya Kupambana na Ufisadi Duniani.

Aliwatahadharisha wawaniaji dhidi ya kutoa taarifa za uongo wanapojaza fomu za uchaguzi.

“Wawaniaji wanafaa wafahamu kuwa hatutatumia maelezo kwenye fomu pekee. Tutaenda hatua moja zaidi na kuanzisha uchunguzi kuhusu madai dhidi yao ikiwemo yale ambayo yametangazwa katika vyombo vya habari,” akaonya.

Wakati wa warsha hiyo, Bw Ruto alisema tume hiyo ishaanza kuweka mikakati ya kufanikisha ushirikiano wake na asasi mbalimbali za serikali, kwa kuwa Wakenya wana haki ya kuwachagua watu wasiokuwa na sifa za uporaji mali katika uchaguzi wa Agosti 2022.

“Tutaendelea kuimarisha utekelezaji wa kitengo cha sheria na kuhakikisha wanasiasa wanaosaka vyeo wamepita mtihani wa maadili. Tunajua kuna wale wajanja watakaolenga kutoa habari za uongo ili waidhinishwe ila nawaonya kuwa tuko nao na tutawakabili,” akasema Bw Ruto.

Pia afisa huyo aliwataka wapigakura nao wawe macho na kuzingatia sifa za wanasiasa wanaosaka uongozi, akisema hiyo itarahisha kazi zaidi kwa EACC na IEBC.

Bungeni, wanasiasa wamekuwa wakipigania marekebisho kwenye kifungu cha Uongozi na Uwazi ili wanasiasa ambao wanakabiliwa na kesi za uhalifu wasiruhusiwe kuwania vyeo mbalimbali.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamepinga marekebisho hayo wakisema kuwa sheria yenyewe inasisitiza mtu hana kosa au hatia hadi pale mkondo wa kisheria utathibitisha hivyo.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Umuhimu wa kutoa zakah katika jamii...

TUSIJE TUKASAHAU

T L