• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
EACC yataka abiria wapige picha polisi fisadi wa trafiki

EACC yataka abiria wapige picha polisi fisadi wa trafiki

NA SIAGO CECE

ABIRIA wameombwa kuripoti visa vyovyote vya maafisa wa trafiki wanaochukua hongo katika barabara kuu za nchini.

Hii ni baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) kutangaza msako mpya dhidi ya polisi wafisadi wa trafiki wanaopokea hongo kutoka kwa madereva wa magari barabarani.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak, alisema hatua hiyo ni ya kuzuia baadhi ya maafisa kupokea pesa kinyume cha sheria kutoka kwa waendeshaji magari, hasa wahudumu wa matatu.

“Vizuizi vya barabarani vimekuwa vituo vya kodi ambapo polisi huchukua hongo waziwazi. Tunataka umma watusaidie katika vita dhidi ya hili kwa sababu sisi kama tume hatuwezi kufanya hivyo peke yetu,” alisema.

Akiongea akiwa Kwale, Bw Mbarak alisema anatarajia raia na wasafiri kufichua na kuripoti visa vya ufisadi, akiwataka kutumia teknolojia kwa kupiga picha na kunasa nambari za usajili wa maafisa wanaoonekana kuchukua hongo kutoka kwa madereva.

“Ikiwa uko kwenye matatu na polisi anaomba hongo kutoka kwa kondakta, wapige picha na uwaambie kuwa umenitumia. Hufai kuruhusu matatu kulipa pesa zozote kwa polisi,” alisema.

Haya yanajiri baada ya tume hiyo kuwakamata maafisa wanne wa polisi wa trafiki eneo la Matuu, kaunti ya Machakos ambao walidaiwa kuitisha hongo kutoka kwa madereva wa magari katika barabara ya Matuu kuelekea Mwingi.

Bw Mbarak alisema changamoto kuu ya kuongezeka kwa hongo kando ya barabara kuu ililetwa na mambo mengi likiwemo suala la ‘ushurui’ ambapo Kamanda wa Polisi wa Kaunti husubiri pesa zake kila wiki kutoka kwa maafisa hao wanaotumwa hadi barabara kuu.

Alisema kuwa taarifa za kijasusi za EACC zimekusanya kwamba maafisa wa trafiki ambao hushindwa kuwapa wakubwa wao pesa za kutosha mwisho wa siku huwa wanahamishwa hadi kwenye barabara kuu isiyo na shughuli nyingi.

Katika Kaunti ya Kwale, wahudumu wa Matatu na Tuktuk walikuwa wameibua wasiwasi juu ya ongezeko la visa ambapo maafisa wanaosimamia barabara hiyo wanahitaji kulipwa angalau Sh100 kwenye vizuizi zaidi ya nne vya barabarani katika maeneo mbalimbali kwenye barabara kuu ya Likoni Lungalunga.

Madereva hao sasa wanaamini uamuzi huu utawasaidia kupata faida zaidi mwishoni mwa siku.

  • Tags

You can share this post!

Utamaduni Dei: Taswira mseto mahasla wakifungua biashara...

AKILIMALI: Huuzia wagonjwa maji moto kujipatia riziki

T L