• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
AKILIMALI: Huuzia wagonjwa maji moto kujipatia riziki

AKILIMALI: Huuzia wagonjwa maji moto kujipatia riziki

Na HEMED ABDALLAH

UKOSEFU wa ajira miongoni mwa Wakenya wengi umechangia pakubwa watu kuibuka na mifumo na mbinu za kila aina katika kutafuta riziki.

Samuel Jengo, 46 ana mke na watoto wanne wanaosoma shule ya msingi.

Baada ya kuangalia huku na kule kuhusu vipi ataweza kujikimu na familia yake, Samuel alianza biashara ya kuchemsha na kuuza maji ya moto kwa wazazi, wagonjwa waliolazwa na hata jamaa wanaowasimamia wagonjwa wao katika Hospitali Kuu ya Pwani maarufu kama Makadara mjini Mombasa.

Huu ni mwaka wake wa tatu akiendesha shughuli hiyo ambayo inawafaa wagonjwa wengi katika hospitali hiyo ya umma.

Katika mahojiano na Akilimali, Samuel, anaeleza kuwa amekuwa akifanya kazi ndogondogo tangu alipomaliza Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Ngenia mnamo 1998.

“Nimekuwa nikiishi kwa kufanya kazi ndogo ndogo ikiwemo uuzaji wa sharubati ili kujikimu kimaisha,” anasema.

Baadaye akiendeleza maisha yake mjini Mombasa aliona fursa ya kibiashara katika uuzaji wa maji moto hawa kwa kinamama wanapojifungua.

“Niliangalia nje ya hospitali kila nimuonae biashara yake ni vyakula na ilhali watu waliolazwa wanateseka ndani ya hospitalii hii ya Makadara kwa ukosefu wa maji moto. Hapo niliona nina nafasi ya kuweka jiko,” anaeleza.

Kulingana naye, kipato chake kilimuwezesha kusukuma gurudumu la maisha kwani amekuwa akiuza lita tano za maji moto kwa Sh50 huku akijua kuwa kuna biashara hasa kwa kinamama wanaojifungua kila siku.

“Lakini hata mimi hupambana na changamoto zangu kwani kuna msimu wa joto jingi ukifika hakuna anunuwaye maji, mara madaktari wakigoma huwa sipati wateja,” anaeleza huku akiongeza kuwa gharama ya kuni ndiyo inayomuumiza kibiashara.

“Kwa siku sikosi elfu zangu mkononi kwa siku na isitoshe nasomesha wanangu na huku nalipa kodi ya nyumba Sh5,000 kila mwezi,” anasema.

Mmoja wa wateja wake, Rose Nyamwera, alisifu biashara hiyo kama inayosaidia wengi hasa wanaolazwa hospitalini Makadara.

“Mimi nina mgonjwa wangu amelazwa hapa Makadara na nimemjua Samuel kwa muda mrefu. Nimesaidika sana kupitia maji moto tunayonunua hapa kwake kwa sababu ikiwa ni ndani ya hospitali, hakuna maji moto,” anaeleza Rose.

Kwa kawaida, jamaa wengi walio na wagonjwa hospitalini wangelazimika kuagiza maji moto kutoka nyumbani au kutafuta mbinu nyingine kila mara wagonjwa wao wakihitaji.

  • Tags

You can share this post!

EACC yataka abiria wapige picha polisi fisadi wa trafiki

Waislamu wakashifu kitabu chenye mchoro wa Mtume unaotaka...

T L