• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
euro hiyo…

euro hiyo…

ROME, Italia

MBIVU na mbichi kuhusu uzuri wa Italia almaarufu Azzurri utajulikana leo itakapoalika Uturuki kwa mechi ya ufunguzi ya Kombe la Bara Ulaya.

Dimba hili la mataifa 24 lilifaa kufanyika 2020, lakini likaahirishwa kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.Italia inatetemesha wakati huu. Inapigiwa upatu kutesa Uturuki ambayo haijapata ushindi dhidi yake katika historia ya mechi baina ya mataifa haya.

Hata hivyo, Uturuki huenda ikajitokeza kuwa mtihani mkali kwa Italia katika mechi hii ya Kundi A kwani imekuwa ikiimarika kwa kasi nzuri.Italia inarejea katika mashindano makubwa baada ya kukosa Kombe la Dunia 2018.

Italenga kuanza kampeni yake vyema nyumbani ugani Olimpico.Mabingwa mara nne wa dunia Italia wana kikosi kilicho na uzoefu mkubwa na pia chipukizi matata. Watakuwa mawindoni kumaliza ukame wa zaidi ya miaka 50 bila taji la Euro.

Waitaliano wako katika orodha ya timu zinazopigiwa upatu kufuzu kwa raundi ijayo.Vijana wa Roberto Mancini wanafukuzia ushindi wao wa nane katika mashindano yote. Ukatili wao pia unadhihirishwa na idadi ya magoli ambayo wamepachika.

Wamejaza wavuni zaidi ya mabao 70 na kufungwa 14 pekee katika mechi zote tangu Mancini achukue usukani.Nayo Uturuki itatumai kumaliza nuksi za kupoteza michuano yake minne ya ufunguzi iliyopita. Inaongozwa na kocha Senol Gunes aliyekuwa usukani wakati timu hiyo ilikamilisha Kombe la Dunia mwaka 2002 katika nafasi ya tatu.

Anaongoza kikosi kilicho na umri mdogo wa wastani miaka 25.Kikosi cha Gunes kimekuwa imara katika idara ya ulinzi. Kilifungwa mabao matatu pekee katika mechi 10 za kufuzu kushiriki Euro 2020.Huku Mancini akiongoza Italia kudumisha rekodi ya kutoshindwa katika mechi 27 zilizopita, Gunes ameshuhudia vijana wake wakipoteza mara tatu pekee katika 26 zilizopita tangu achukue usukani tena 2019.

Uturuki inapigiwa upatu kupata tiketi ya 16-bora kutoka kundi hili ambalo pia linajumuisha Wales na Uswizi.Baadhi ya wachezaji walio na uwezo mkubwa wa kuamua mwekeleo wa mechi hii ni mshambuliaji Mwitaliano Ciro Immobile na mwenzake kutoka Uturuki, Burak Yilmaz.

Kipa Gianluigi Donnarumma anayewaniwa sokoni wakati huu kama mpira wa kona pia atakuwa kiungo muhimu kwa Italia. Mara ya mwisho Italia ilitwaa ubingwa wa mashindano haya ilikuwa 1968 ilipokuwa mwenyeji wa dimba hili.

Katika mechi 10 ambapo mataifa haya yamekutana, Italia inajivunia ushindi mara saba na kupiga sare tatu.Mataifa 24 yanashiriki kipute hiki maarufu Euro ambacho tuzo yote imepunguzwa kutoka Sh48.5 bilioni hadi Sh43.3 bilioni kutokana na janga la covid-19.

  • Tags

You can share this post!

ICC yataka mibabe sita wa vita Sudan wasalimishwe

Mungu hutoa riziki kwa waja wake wanaoomba na kuitafuta kwa...