• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Everton wapepeta Burnley na kutinga nne-bora EPL

Everton wapepeta Burnley na kutinga nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

EVERTON walitinga ndani ya mduara wa nne-bora kwa alama 10 sawa na Manchester United, Chelsea na Liverpool baada ya kutoka nyuma mnamo Jumatatu usiku na kupepeta Burnley 3-1 uwanjani Goodison Park.

Michael Keane aliwarejesha Everton mchezoni katika dakika ya 60 baada ya Ben Mee kuwaweka Burnley uongozini katika dakika ya 53. Mechi hiyo ilikuwa ya 200 kwa Mee kuchezea Burnley almaarufu ‘The Clarets’.

Andros Townsend alipachika wavuni bao la pili la Everton katika dakika ya 65, sekunde chache kabla ya Demarai Gray kushirikiana vilivyo na Abdoulaye Doucoure kuzamisha chombo cha wageni wao.

Chini ya kocha Rafael Benitez, Everton kwa sasa hawajashindwa katika mechi nne za ufunguzi wa kampeni za Ligi Kuu ya Uingeeza (EPL) msimu huu.

Kikosi hicho kilichoagana na mkufunzi Carlo Ancelotti mwishoni mwa muhula wa 2020-21, kilianza kampeni za msimu huu kwa kushinda Southampton 3-1 kabla ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Leeds United katika mechi ya pili kisha kucharaza Brighton 2-0 katika mchuano wa tatu.

Everton walisakata mechi hiyo bila kujivunia huduma za fowadi matata Dominic Calvert-Lewin ambaye atasalia mkekani kwa kipindi cha wiki mbili zijazo kuuguza majeraha ya paja na kidole cha mguu.

Kufikia sasa, Burnley hawajashinda mechi yoyote ligini na wanashikilia nafasi ya 18 kwa alama moja sawa na nambari 19, Newcastle United. Limbukeni Norwich City wanavuta mkia bila pointi yoyote.

Townsend na Gray wanazidi kuwa tegemeo kubwa la Everton tangu wajiunge na kikosi hicho almaarufu ‘The Toffees’ mwishoni mwa msimu wa 2020-21 kwa jumla ya Sh265 milioni pekee. Wawili hao walishirikiana vilivyo na fowadi Richarlson Andrade katika mfumo wa 3-4-3 ambao unazidi kukumbatiwa na Benitez.

  • Tags

You can share this post!

Anaamini talanta ya kuigiza itasaidia wengi miaka ijayo

Madaktari bandia washtakiwa kudunga watu chanjo bandia ya...