• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Familia yalilia haki baada ya mwana wao kuuawa kwa risasi wakati wa maandamano ya Azimio

Familia yalilia haki baada ya mwana wao kuuawa kwa risasi wakati wa maandamano ya Azimio

NA MERCY KOSKEI

FAMILIA ya mwanamume aliyeuwawa katika eneo la Stima line, Kaunti ya Nakuru Jumatano Julai 19, 2023 wakati wa maandamano kushinikiza serikali kushusha gharama ya maisha inataka haki na waliohusika kukamatwa.

Benjamin Indi, 32, mwendesha bodaboda anadaiwa kupigwa risasi na polisi wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa polisi.

Kulingana na ndugu ya marehemu Bw Christopher Heman, kabla ya kuuwawa Indi aliondoka nyumbani na kuelekea katika steji ya bodaboda ambapo alikuwa akiendeshea shughuli zake kwa miaka mitatu, mita chache kutoka alikofariki.

Hata hivyo, saa chache baadaye alipokea simu ya huzuni kutoka kwa jirani yake akimjulisha kuwa kaka yake ameuawa kwa kupigwa risasi na kuwa anatakiwa kufika eneo la tukio.

Jambo hilo lilimfanya kuwapigia marafiki na wafanyakazi wenzake simu ambapo walimthibitishia kuwa Bw Indi alipigwa risasi.

Hata hivyo, alipowasili tayari ulikuwa umeondolewa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Nakuru City.

Benjamin Imbi, 32, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya Azimio jijini Nakuru. Picha|BONIFACE MWANGI
32-year-old Benjamin Imbi who was shot dead by police during anti-government protest on July 19, 2023 at Stima Line in Nakuru City. BONIFACE MWANGI/NATION

Kulingana na Bw Hemman, kakake alipata jeraha la risasi kwenye jicho lake la kulia.

Bw Heman alieleza Taifa Leo Dijitali kuwa kwa sasa wametembelea afisi ya chifu ili kupewa kibali cha kuanzisha mipango ya mazishi.

“Sina uhakika alikuwa miongoni mwa waandamanaji, alikuwa akifanya kazi eneo hilo. Huenda alikuwa hapo au alinaswa katika mapigano kati ya polisi na waandamanaji. Sababu za kupigwa risasi zingali kitendawili kwetu na tunachotaka kama familia ni haki,” alisema.

Alimkumbuka marehemu kuwa kijana mchapakazi ambaye siku zote alijitahidi kutunza familia yake licha ya kutengana na mkewe miaka miwili iliyopita.

Bi Elizabeth Andami, dadake, alikubuka mara ya mwisho kuwa na nduguye akisema kuwa alifika nyumbani kwake eneo la Pondamali siku ya Jumapili.

Alisema kuwa walikula chakula cha jioni pamoja kabla ya kuondoka huku akiahidi kwamba angerejea Jumanne jioni.

Elizabeth Andami akitazama picha ya ndunguye mkubwa na wa pekee Benjamin Imbi ambaye aliuwawa na polisi baada ya kupigwa risasi mnamo Julai 19, 2023 wakati wa maandamano Azimio Nakuru. Picha|BONIFACE MWANGI

Hata hivyo, siku ya Jumanne Imbi alimpigia simu na kumwarifu kuwa ameshikika kazini na kuwa atafika siku ya Jumatano jambo ambalo halikufanyika.

“Wanataka tufanye uchunguzi wa maiti na tunajua sababu ya kifo chake. Hatuna pesa za kumwaga, badala yake tunataka kuzitumia kwa gharama ya mazishi. Sisi ni yatima, hatuna mtu wa kumtegemea,” alisema huku akitokwa na machozi.

Familia hiyo kwa sasa inaomba wasamaria wema kuwasaidia kusafirisha mwili nyumbani kwao Kaunti ya Siaya kwa minajili ya mazishi.

 

  • Tags

You can share this post!

Miguna Miguna akosa kwenye orodha ya uteuzi wa DPP

Makahaba na washirika wa kanisa Thika wazozania jengo la...

T L