• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Makahaba na washirika wa kanisa Thika wazozania jengo la kazi 

Makahaba na washirika wa kanisa Thika wazozania jengo la kazi 

Na MWANGI MUIRURI 

MAKAHABA wanaotegea wateja katika baa moja Mjini Thika wamelalamikia hatua ya waumini wa kanisa linalotaka wazimwe kuhudumu Jumapili.

Wanawake hao ambao huhudumu katika baa la McGeorge lililoko katika barabara ya Kwame Nkurumah, wametaja mwito huo kama wa ubinafsi.

Mtafaruku huu umetokana na hali kwamba kanisa hilo la Wordfest Chapel International linaloongozwa na pasta Kelvin Macharia liko katika jengo hilo.

“Kila Jumapili tunatatizika sana kuingia kanisani kwa kuwa wanawake hao huwa nusu uchi, mikononi wakiwa na vikombe vya pombe na wengine mipira ya kondomu wakishikashika wanaume nje ya madhabahu yetu,” akasema Bi Esther Karuga, muumini.

Pasta Macharia katika ukurasa wake wa Facebook unaonyesha kwamba kanisa hilo hutamatisha ibada mwendo wa saa saba, waumini wake sasa wakiwataka makahaba hao kuzima biashara zao hadi saa nane mchana kuwapa nafasi ya kufunga kanisa.

Kuingia katika kanisa hilo, ni lazima upitie ndani ya baa, kisha lojing’i na hatimaye upitane na wateja na wauzaji wa ngono wakiteremka au wakipanda wakiongea lugha inayoambatana na biashara hiyo.

Waumini hao sasa wanaitaka serikali ya Kauniti ya Kiambu kuzuia wanawake hao kuhudumu katika jengo hilo kila Jumapili ili kuwapa washirika nafasi ya kuabudu bila kutatizwa na aibu, kelele na harufu za ngono.

Hata hivyo, msemaji wa wanawake hao Bi Virginia Ngugi alisema kwamba “kanisa hilo ndilo lilitafuta makao yake kwenye himaya yetu”.

Bi Ngugi alidai kwamba “hao polisi wanaotakiwa watufurushe bado kunao wateja wetu na hata baadhi ya waumini wa kanisa hilo huabudu nasi kibiashara”.

Alisema hatua ya kuwafurusha kutoka jengo hilo itapingwa “hata ikiwa itabidi tuandamane mitaani”.

Naibu Kamishna wa Thika Magharibi Bi Philomena Nzioki alisema kwamba “shida tuliyo nayo kuu ni wanaotoa leseni za mabaa kwa kuwa ndio wameweka mazingara hayo ya mitafaruku”.

Bi Nzioki aliteta kwamba “mkono wa sheria umefungwa na leseni hizo, kilichobakia sasa kikiwa ni wote walio na pingamizi kuhusu kuwepo kwa wanawake hao ndani ya jumba hilo la kanisa waandike barua rasmi ya kulalamika”.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Familia yalilia haki baada ya mwana wao kuuawa kwa risasi...

Sabina Chege alalamikia bunge kuwa na wezi wa simu

T L