• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Gavana, Naibu wake bado hawapikiki chungu kimoja Mashujaa Dei ikikaribia

Gavana, Naibu wake bado hawapikiki chungu kimoja Mashujaa Dei ikikaribia

NA VITALIS KIMUTAI

Gavana wa Kericho Erick Mutai na Naibu wake Fred Kirui bado hawajazika tofauti zao mwaka mmoja baada ya kuingia mamlakani huku juhudi za kuwapatanisha zikigonga mwamba mara mbili.

Tofauti zao zinaendelea huku kaunti hiyo ikitarajiwa kufanikisha uandalizi wa sherehe za kuadhamisha Mashujaa Dei mwaka huu.

Mzozo wao unatokana na mkataba wao wa kabla ya uchaguzi mkuu wa kugawana mamlaka kwa asilimia 60-40 ambao Bw Kirui analaumu mkubwa wake kwa kukiuka.

Kwa mwaka mmoja uliopita, wawili hao wamekuwa wakizozana huku wakipatanishwa mara mbili na kukosana tena jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa ajenda ya maendeleo na umoja wa serikali ya kaunti.

Naibu Rais Rigathi Gachagua hajatimiza ahadi yake aliyotoa mwezi mmoja uliopita ya kualika Dkt Mutai na Bw Kirui Nyeri kwa kikao cha maridhiano.

Bw Gachagua alifichua akiwa Londiani mnamo Septemba 8, wakati wa mazishi ya wakili Vincent Mutai, mwanawe Mbunge wa Kipkelion Mashariki Joseph Cherorot kwamba Rais William Ruto anasikitishwa na mzozo kati ya gavana huyo na naibu wake.

“Mimi na Rais tumesikitishwa na mizozo katika kaunti ya Kericho. Hivi majuzi Rais nusura afute maandalizi ya Mashujaa Dei katika kaunti ya Kericho, lakini nilimshawishi na akaruhusu yaendelee. Suala hilo ni zito,” Bw Gachagua alisema.

Bw Gachagua alisema kuwa angewaita Dkt Mutai na Bw Kirui hadi Nyeri kwa kikao cha maridhiano, na ikiwa hawatakubali kuzika tofauti zao, wangekabiliwa na hatari ya kuondolewa afisini.

“Ikiwa hamtatii wito wa wananchi wa kuungana na kuwafanyia kazi, basi hatutakuwa na chaguo ila kuwaponda kisiasa…Nitaenda kwenye vituo vya redio vya lugha za kienyeji (vinatangaza kwa lugha ya Kalenjin) na kutangaza tumewaachia wananchi wawasukume nje,” Bw Gachagua alisema.

  • Tags

You can share this post!

Tineja mmoja kutoka Ganze auawa kwa kukatwa shingoni

Cherargei ashambulia kamati ya NADCO kwa kukataa kusikiliza...

T L