• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Hakimu aliyekataa kuagiza baba mzazi alipie mahitaji yote ya watoto ajitetea

Hakimu aliyekataa kuagiza baba mzazi alipie mahitaji yote ya watoto ajitetea

TITUS OMINDE na FRIDAH OKACHI

HAKIMU mkuu Christine Menya amejitetea kwa kukataa kuagiza baba alipe malezi yote katika kesi iliyokuwa ikimhusisha mama na watoto wawili. Uamuzi huo ulisababisha mama huyo kupandwa na hasira kortini na kuzua vurumai.

Katika video hiyo iliyowekwa kwenye ukurasa wa Nation.Africa, mama huyo mwenye hasira alikataa uamuzi uliotolewa Oktoba 6, 2023 kuhusu kutunza watoto wawili na mpenziwe ambaye ni mwalimu mkuu.

Mwanamke huyo, 25, aliukataa uamuzi wa mahakama baba ya watoto hao, wenye umri wa miaka 5 na miezi 9, kulipia karo ya shule na kumpa mama Sh5,000 kila mwezi.

Mahakama ilisema kuwa watoto hao walizaliwa nje ya ndoa kati ya mlalamishi na mshtakiwa ambaye ana familia nyingine.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani Mei, 2023 na kuamuliwa Oktoba 6, 2023.

Mama huyo mwenye hamaki, alishtumu mahakama kwa kukosa kumshinikiza baba watoto kutekeleza majukumu yote kwa wanawe wawili. Mlalamishi alitarajia mahakama kuamrisha kutimiza mahitaji yote ya watoto hao ikiwa ni chakula, mavazi, matibabu na malazi.

 “Hii si sawa, na sitakubaliana na uamuzi huo. Je, kuhusu karo ya shule ya watoto hawa, haswa yule mdogo ambaye bado hajaanza shule?” aliuliza wakati wa kesi kuamuliwa.

Mahakama ilipatwa na wakati mgumu wa kumshawishi kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo ambao haukumridhisha.

Hakimu mkuu Christine Menya alisema uamuzi wake ni kuhakikisha maslahi ya watoto yanalindwa kwa uamuzi bora.

Alisisitiza uamuzi wake ulikuwa wa haki na kumpa kipaumbele mlalamishi, kulingana na sheria za watoto.

“Kulingana na kifungu 81 cha Sheria ya watoto Nambari 8 ya 2001, inafafanua ulezi wa mtoto kuweza kuwa na haki nyingi na wajibu wa mzazi kuhusiana na umiliki wa mtoto,” alieleza Hakimu Mkuu.

Kulingana na Hakimu Menya, uamuzi wake ulizingatia sheria ya watoto ya mwaka 2001, ambayo inaamuru mtu kufanya malipo kwa ajili ya malezi ya mtoto.

“Wakati wa kutuma ombi la malezi, mlalamishi anatakiwa kuwasilisha hati kiapo kwa njia inayoeleza matumizi ya mtoto pamoja na kutoa uthibitisho wa matumizi. Hivyo ndivyo ilitokea katika kesi hii,”alisema Hakimu Menya.

Hakimu  alisistiza hajutii uamuzi huo, akimtaka mlalamishi kukata rufaa kwa mahakama ya juu zaidi.

Kulingana na Sheria wakati wa kutoa uamuzi katika mahakama inayohusisha watoto, mahakama huzingatia mapato ya mtu, mali na vitu vingine vinavyoonekana kuwa na thamani.

Sheria huzingatia mahitaji ya kifedha ya mtoto na hali ya sasa ya mtoto miongoni mwa mambo mengine.

Kinaya ni kuwa baada ya uamuzi huo na mafadhaiko kutoka kwa mama huyo, wawili hao ambao ni mlalamishi na mshtakiwa waliondoka mahakamani kwenye gari moja.

  • Tags

You can share this post!

Wamuchomba asimulia alivyochapwa na babake kwa kutokea...

Maisha kuzidi kuwa magumu stima ikiongezwa bei

T L