• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wamuchomba asimulia alivyochapwa na babake kwa kutokea gazetini alipoibuka bora KCPE

Wamuchomba asimulia alivyochapwa na babake kwa kutokea gazetini alipoibuka bora KCPE

NA FRIDAH OKACHI

MBUNGE wa Githunguri Gathoni Wa Muchomba amefichua baadhi ya changamoto alizopitia akikua, mojawapo ikiwa adhabu kali kwa sababu ya picha yake kuchapishwa kwenye gazeti.

Bi Wa Muchomba alisema babake alimtwanga licha ya kupita mtihani wa kitaifa wa KCPE.

Kulingana naye, mzazi wake huyo wa kiume alikuwa raibu wa pombe.

“Siku moja alipofika nyumbani baada ya kazi, aliamua kunishukia kwa vita. Nakumbuka, alipitia katika maduka ya mtaani, watu wakamuonyesha picha yangu iliyokuwa imechapishwa kwenye gazeti. Aliishia kuniadhibu ajabu,” Wa Muchomba akafichua, kupitia mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini.

Cha kushangaza kulingana na mbunge huyo ambaye ni mwanachama wa United Democratic Alliance (UDA), na ambaye amepata umaarufu kutokana na ujasiri wake kutetea mwananchi wa kawaida, alisema babake hakuwa anafahamu darasa alilokuwa.

“Baba hakuwa anajua nipo Darasa la Nane…Kila wakati alikuwa akiniuliza darasa nililokuwa,” Bi Wamuchomba alisimulia.

Mwanasiasa huyo ambaye kabla ya kuchaguliwa mbunge Githunguri Agosti 2022 alihudumu kama Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kiambu, alifunguka hayo wakati akizungumzia changamoto ambazo familia nyingi hupitia kutokana na kero ya pombe.

Usiku wa tukio la kupigwa na babake, familia yake nusra ilale nje.

Alisema baba aliifukuza wakati mvua ikiendelea kunyesha.

“Ilibidi tusubiri alale ili turejee nyumbani,” alisema mtangazaji huyo wa zamani.

Gathoni Wamuchomba amekuwa balozi wa malezi bora kwa watoto, akiwataka wazazi kuwajibika.

Mbunge huyo vilevile amekuwa akikosoa mpango wa serikali ya Kenya Kwanza kupambana na kero ya pombe haramu, dawa za kulevya na mihadarati eneo la Mlima Kenya, akisema operesheni hiyo itafanikishwa iwapo kiini kitaangaziwa.

Naibu Rais Rigathi Gachagua ndiye anaongoza operesheni hiyo, na Bi Wamuchomba anaamini ukosefu wa ajira kwa vijana ukiangaziwa kikamilifu utasaidia kuzima kero ya pombe si tu eneo la Kati bali kote nchini.

  • Tags

You can share this post!

Baiskeli zaendelea kutumika Nakuru licha ya kupandishwa...

Hakimu aliyekataa kuagiza baba mzazi alipie mahitaji yote...

T L