• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Akina dada 500 wakongamana Thika kupewa hamasisho la kujiendeleza kibiashara

Akina dada 500 wakongamana Thika kupewa hamasisho la kujiendeleza kibiashara

Na LAWRENCE ONGARO

AKINA dada 500 walikongamana mjini Thika kupata hamasisho kuhusu biashara.

Idadi hiyo inawakilisha jumla ya akina dada 10,000 walio na ari ya kujiendeleza kibiashara kutoka katika maeneo yote ya Kaunti ya Kiambu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alijitolea kuwahamasisha kuhusu uwekezaji wa fedha kupitia mpango wa J-Hela ambao pia unatoa mikopo kwa vikundi vya watu.

Mbunge huyo aliwahimiza vijana kuwa mstari wa mbele kukumbatia biashara kwa lengo la kujiendeleza zaidi.

“Hakuna haja ya kutegemea ajira kila mara kwa sababu biashara inaleta faida kubwa na pia ni njia bora ya kufanya maendeleo ya haraka,” alifafanua mbunge huyo.

Aliwarai akina dada hao kufanya hima na kujiweka kwa makundi ya watu kumi au zaidi ili waweze kupata mikopo ya haraka kupitia mpango wa J-Hela.

Alitoa mfano wa wahudumu wa bodaboda kutoka Kiganjo, Makongeni, Thika ambao walijiunga kwa vikundi miaka michache iliyopita na sasa wao ndio wamiliki ya jumba la orofa nne na wanapata kodi kutoka kwa wanaoishi katika vyumba vya jumba hilo.

“Hiyo ni hatua kubwa sana kwa sababu walianza kuweka kwenye hazina yao Sh100 kila siku kwa kila mmoja na baada ya muda fulani walipokea mkopo kutoka kwa mpango wa J-Hela, ambapo walifanikiwa kujinunulia kipande cha ardhi na wakaanza kujenga jumba la orofa nne polepole,” alisema mbunge huyo.

Kwa muda wa zaidi ya miezi sita, mbunge huyo amekuwa akihamasisha wakulima na wakazi wa kaunti ya Kiambu jinsi ya kuendesha biashara hasa kwa kujiweka kwa makundi.

Mmoja wa akina dada waliohudhuria hafla hiyo Sylvia Kitavi, alipongeza juhudi za Bw Wainaina za kuwahamasisha ili kujitegemea kibiashara.

“Sisi akina dada tumefurahia ujumbe tuliopata kutoka kwa Bw Wainaina kwa sababu tumepata maarifa mazuri ya kutupeleka mbele,” alifafanua mwanadada huyo.

Alisema wakati huu wao akina dada wa kutoka mashinani hawatakubali kuyumbishwa na maswala ya siasa lakini wako na maono ya kujiendeleza kibiashara.

Baadhi ya akina dada waliohudhuria kongamano la hamasisho la kibiashara. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mary Wanjiku, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema wamepongeza hatua hiyo kwa sababu watajiunga kwa vikundi ili waweze kujiendeleza zaidi na biashara zao.

Alisema tayari mbunge huyo wa Thika “ametufunza jinsi ya kuvua samaki badala ya kutupatia samaki wa kula.”

  • Tags

You can share this post!

Covid: Kagwe aapa kupuuza uamuzi wa korti kuhusu chanjo

Kingi ataka serikali kuu ikarabati daraja

T L