• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Helikopta iliyokuwa imembeba Raila yaanguka punde baada ya kumshukisha

Helikopta iliyokuwa imembeba Raila yaanguka punde baada ya kumshukisha

Na CAROLINE WAFULA

NDEGE iliyokuwa imembeba kinara wa ODM Raila Odinga kwenda Kaunti ya Siaya, Jumapili wakati wa ziara ya rais Uhuru Kenyatta, ilianguka muda mfupi baada ya kumshukisha na ujumbe wake wa watu wanne.

Helikopta hiyo aina ya Bell 407, yenye usajili 5Y-PSM ilikuwa imemshukisha Bw Odinga katika shule ya msingi ya Kudho eneo la Gem. Ilijaribu kupaa ili iondokee ndege nyingine lakini ikashindwa.

Baada ya mkasa huo wa mwendo wa saa kumi na nusu alasiri kijijini Usenge, Msemaji wa Bw Odinga, Dennis Onyango alisema kinara huyo wa ODM yuko salama.

Bw Odinga alikuwa amempokea Rais katika uwanja wa Kimataifa wa Kisumu mwendo wa saa tisa, kabla ya kuondoka kwa helikopta tofauti kuelekea Siaya, ambako Rais alizindua barabara ya Wagai-Akala.

“Rubani na abiria wake wanne walipata majeraha madogo. Bw Odinga aliendelea vyema na ratiba ya shughuli zake na Rais,” akasema Bw Onyango.

Ajali hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Akala na Kapteni Julius Mwambanga wa kampuni ya Pieniel Air iliyokuwa ikimsafirisha Bw Odinga.

You can share this post!

Ruto sasa aingia vijijini akilenga kuvumisha UDA

Hasara, hofu ndovu wakivivamia vijiji