• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Hofu mvua ya El Nino ikinukia huku serikali ikijikokota

Hofu mvua ya El Nino ikinukia huku serikali ikijikokota

Na STANLEY NGOTHO_

WAKENYA sasa wana wasiwasi huku serikali ikikosa kuonyesha dalili za kujitayarisha kukabili athari za mvua ya El Nino inayotarajiwa kuanza Oktoba.

Hii ni baada ya Idara ya Hali ya Hewa nchini kutangaza uwezekano wa mvua wa El Nino kugonga Kenya kati ya Oktoba na Desemba.

Hata hivyo, kimya cha serikali na kukosa kutoa hatua zitakazochukuliwa kukabiliana na athari za El Nino sasa kinawatia Wakenya wasiwasi.

Kulingana na ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame, BiRebecca Miano, alisema kuwa serikali ya kitaifa inafaa kuwa na jumla ya Sh33 bilioni ili kukabiliana na athari za mvua ya El Nino.

Serikali ya Kaunti ya Kajiado, kama kaunti nyingi kwa sasa haijajiandaa kukabiliana na athari za El Nino.

“Tuna matumaini kuwa fedha zitakazotolewa na serikali ya Kitaifa zitatufikia,” akasema afisa mkuu katika kaunti hiyo.

Hata hivyo, Taifa Leo haikuweza kumfikia waziri anayesimamia masuala ya mazingira katika kaunti hiyo kutoa maoni yake.

Bw Kennedy Parmeres, 54, kutoka Loitok tok katika Kaunti Ndogo ya Kajiado kusini, alisema kuwa huenda eneo hilo likaathirika zaidi ikiwa El Nino itagonga eneo hilo kama ilivyotokea mwaka wa 1997/1998.

Bw Parmeres alisema kuwa hatua ya kukata miti ovyo ovyo katika eneo hilo huenda ikafanya athari za mvua ya El Nino kuwa mbaya zaidi.

“Huenda ikawa mbaya zaidi mwaka huu. Huenda mashamba yetu yakaathiriwa kama ilivyofanyika miaka ya hapo nyuma. Barabara ya Ilasit-Taveta huenda ikafungwa kwa muda wakati wa mvua,” akasema Bw Parmeres.

Aliyekuwa Seneta wa Kajiado, Bw Peter Mositet, alisema kuwa wengi wataangamia ikiwa mvua hiyo itashuhudiwa nchini.

Bw Mositet alisema vitengo vilivyogatuliwa vinapaswa kuwa na uwezo wa kutenga baadhi ya fedha kutoka kaunti ili kushughulikia masuala kama hayo.

“Ni wazi kuwa baadhi ya kaunti hazijajipanga kukabiliana na athari za mvua. Serikali inafaa kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kupanda miti,” akasema Bw Mositet.

El Nino hutokea viwango vya joto baharini vinapopanda hasa katika Bahari ya Pacific na kubadilisha hali ya hewa katika nchi mbalimbali ulimwenguni.

Hali hii huchangia mvua kubwa ukanda wa Afrika Mashariki hasa kuanzia Oktoba-Novemba na Desemba.

  • Tags

You can share this post!

MKU yashirikiana na IUM ya Namibia kwa maswala ya afya

Mbunge wa Kisumu Mashariki atishia kwenda korti kusimamisha...

T L