• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Ichung’wah akana kuhusika na uvamizi wa shamba la Uhuru

Ichung’wah akana kuhusika na uvamizi wa shamba la Uhuru

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah amekana madai ya kuhusika na uvamizi wa shamba linalomilikiwa na familia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika eneo la Ruiru, Kiambu.

Akiongea na wanahabari Jumanne katika majengo ya bunge, Bw Ichung’wah hata hivyo, alisema kuwa yu tayari kuchunguzwa na polisi kuhusiana na kisa hicho.

“Sina habari zozote kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, polisi wanajua kwangu Kikuyu, pia wanajua afisi hapa bungeni na huko katika eneobunge langu. Ikiwa kuna habari zozote ambazo wanazitaka kutoka kwangu, niko tayari kushirikiana nao,” akasema mbunge huyo wa Kikuyu.

Bw Ichung’wah ambaye alikuwa ameandamana na mwenzake wa Seneti Aaron Cheruiyot na wabunge wengine wanane wa UDA, aliwataka polisi kufanya uchunguzi kuhusu uvamizi huo ili kuwatia mbaroni wahusika wote.

“Ni kazi ya polisi kuchunguza kile kilichotendeka. Mimi niko tayari kuwasilisha habari zozote endapo nitaulizwa kufanya hivyo,” akasema.

Hata hivyo, Bw Ichung’wah alidai kuwa uvamizi wa shamba hilo linalojulikana kama Northland City na kampuni ya gesi ya Spectre East Africa Limited ulipangwa na Bw Kenyatta na Raila Odinga ili kuwaharibia jina yeye na viongozi wengine wakuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

“Huu unavamizi ulifanywa ili kuthibitisha madai ya Bw Odinga kwamba mimi, Naibu Rais Rigathi Gachagua na Ndindi Nyoro tulipanga kukodi vijana kusababisha vurugu wakati wa maandamano yao. Ningependa kusema kusema kuwa siku ambayo Raila anadai nilikuwa kwenye mkutano wa kupanga ghasia, ukweli ni kwamba nilikuwa nyumbani kwangu Kikuyu,” akaeleza.

Bw Ichung’wah alishangaa ni jinsi gani shamba la Northland City lingevamiwa na wahuni ilahi linalindwa na maafisa wa polisi usiku na mchana.

“Swali langu ni je, maafisa hawa walikuwa wapi wakati wa uvamizi huo? Nahisi kuna Wakenya wanachezewa shere hapa,” Bw Ichung’wah akasema.

Madai ya Bw Ichung’wah yanajiri baada ya kanda ya video kuzunguka mitandaoni ikimwonyesha akitisha kuwa “tatavamia mashamba ya Uhuru na kugawi wananchi wasio na mashamba.”

Bw Ichung’wah anadaiwa kutoa matamshi hayo mnamo Jumamosi 11/3/2023 katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kianyaga, kaunti ya Kirinyaga.

Alitoa matamshi hayo wakati wa hafla ya wanafunzi wa zamani wa shule, akiwemo Naibu Rais Bw Gachagua.

Bw Ichung’wah alimsuta Bw Kenyatta kwa kile alichodai ni hatua yake ya kudhamini maandamano ya Azimio chini ya uongozi wa Bw Odinga.

Wahuni waliovamia shamba la Northlands City la ukubwa wa ekari 11,000, walikuwa wamejihami kwa misumeno, mapanga na silaha nyingine butu. Walitumia misumeno hiyo ya injini kukata miti katika shamba hilo.

Wahalifu hao pia walichukua zaidi ya kondoo 1,400 ambao hufugwa katika sehemu ya shamba hilo.

  • Tags

You can share this post!

Kenya inaelewa lugha ya nishati safi – Ruto

Raila sasa afokea nchi za kigeni

T L